Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Wakala ya Serikali Mtandao.

Miundombinu

Miundombinu

2015-11-09

Katika jitihada za kuondoa urudufu, kupunguza gharama na kuongeza ubora wa huduma kwa umma, Serikali inaweka na kuboresha miundombinu ya TEHAMA salama na ya uhakika ambayo itaziwezesha taasisi za umma kushirikiana katika matumizi ya rasilimali hizo. Miundombinu hiyo ni pamoja na Mfumo wa Barua Pepe Serikalini (GMS), Mtandao wa Mawasiliano Serikalini (GovNet), Vituo vya Kitaifa vya Data (Data Centre) na Masafa ya Intaneti (Government International Bandwidth) na Vitumi vya Mkononi (Government Mobile Platform).

Mfumo wa Barua Pepe Serikalini

Mfumo huu unasaidia kurahisisha mawasiliano kwa njia ya barua pepe kwa taasisi za Serikali na kuongeza usalama wa taarifa zinazosafirishwa kwa mfumo huu. Katika kipindi hiki, taasisi 210 zinatumia mfumo huu na taratibu za kuziunganisha taasisi zilizobaki kwenye mfumo huu zinaendelea.  Aidha, katika kuhakikisha mfumo huu unabadilishana taarifa na mifumo mingine ya Serikali, mfumo huu umeunganishwa na Mfumo Shirikishi wa Rasilimaliwatu na Mishahara (HCMIS).

Mtandao wa Serikali (GovNet)

Taasisi zote za umma zinaunganishwa kwenye mtandao mmoja wa mawasiliano ambao ni salama na wenye gharama nafuu. Mtandao huu una lengo la kuziwezesha taasisi za umma kuwa na mawasiliano ya kielektroni (data, sauti na video) ya ndani. Hadi sasa, Wizara, Idara na Wakala 72 zimeunganishwa na taasisi 50 zinatumia huduma zinazopatikana katika mtandao huu. Aidha taasisi 77 za Mamlaka ya Serikali za Mitaa zinatarajiwa kuunganishwa kwa mwaka fedha 2015/16.

Vituo vya Kuhifadhi Mifumo na Data

 Serikali imetenga asilimia 25 ya Kituo Kikuu cha Data cha Taifa kwa ajili ya matumizi ya Serikali. Aidha, ujenzi wa vituo vidogo vya kuhifadhi mifumo (Mini Data Centers) kwa ajili ya matumizi ya Serikali unaendelea. Vituo hivi vitatumika kama sehemu ya kujikinga na majanga (Disaster Recovery Site) kwa mifumo na data zilizohifadhiwa kwenye Kituo Kikuu.

Masafa ya intaneti (Internet Bandwidth)

Serikali imenunua haki miliki za kutumia (Indefeasible Right of Use (IRU)) masafa ya intaneti ya kiasi cha 1.55 Gbps kwa muda wa miaka 10 kuanzia mwaka 2013.  Hadi sasa jumla ya taasisi za umma 160 zimeunganishwa katika masafa haya.

Huduma za Serikali kwa Kutumia Simu za Mkononi

Katika kuboresha matumizi ya fursa zitokanazo na Simu za Mkononi, Wakala imeongeza huduma zitolewazo kupitia namba za USSD pamoja na kuongeza aina tatu (3) ya huduma zinazotumia namba hizo. Aidha, Wakala imeratibu ugawaji wa  namba za USSD kwa taasisi 10.  Namba hizo zinaanzia *152*00# hadi *152*99#.

 Pia, Wakala imetengeneza Mfumo wa Huduma ya Ujumbe Mfupi wa Maandishi kwa Simu za Mkononi (GovSms) kwa lengo la kuziwezesha taasisi za Serikali kuwahudumia wananchi kwa urahisi, haraka, usalama na gharama nafuu kupitia simu zao za mkononi. Mfumo huu unaziwezesha taasisi za Serikali kutuma ujumbe kwa mwananchi mmoja mmoja (Quick sms), makundi (Group sms) na kwa wingi (Bulk sms) kwa wakati mmoja. Mpaka sasa, huduma hii ya GovSMS inatumiwa na taasisi za serikali 28 kutoa huduma ya ujumbe mfupi wa maandishi kwa umma