Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Wakala ya Serikali Mtandao.

Huduma Mtandao

Huduma Mtandao

Ili kuhakikisha kuwa jamii inapata taarifa na huduma mbalimbali kwa njia ya mtandao kwa wakati, uwazi, urahisi na kwa gharama nafuu, Wakala ya Serikali Mtandao Wakala imechukua hatua mbalimbali za kupanua wigo na kuboresha njia za utoaji wa huduma mtandao (Service Delivery Channels). Maeneo yaliyolengwa na hatua hizi ni pamoja na Tovuti Kuu ya Serikali, Tovuti Kuu ya Ajira na Tovuti Kuu ya Takwimu Huria.  

Tovuti Kuu ya Serikali

 Tovuti Kuu ya Serikali (http://tanzania.go.tz/ ambayo ni dirisha moja la utoaji wa huduma na taarifa kwa umma imeendelea kuboreshwa. Maboresho yaliyofanyika ni kuongeza eneo jipya la  Huduma ya Matangazo inayotoa fursa kwa Taasisi za umma kutangaza huduma zao  pamoja na kuhuisha eneo la ‘Nifanyeje’ kwenye tovuti hiyo. Maudhui ya Tovuti Kuu hiyo yanapatikana kwa lugha ya Kiingereza na Kiswahili na yamegawanyika katika sehemu kuu saba ambazo ni Serikali, Wananchi, Taifa Letu, Biashara, Sekta, Mambo ya Nje na Nifanyeje

Tovuti Kuu ya Ajira

 Tovuti Kuu ya Ajira http://portal.ajira.go.tz/ajira/  ni dirisha kuu la kutangaza nafasi za kazi Serikalini, ambapo wanaotafuta kazi wanapaswa kuweka taarifa zao mara moja kwenye tovuti hiyo na pindi zinapotokea nafasi za kazi wanataarifiwa kupitia barua pepe au simu ya mkononi. Maboresho yaliyofanyika kwenye tovuti hii katika kipindi hiki ni kuiwezesha Sekretariati ya Ajira kuchopoa orodha ya waombaji wote na wasifu wao pamoja na kuwawezesha watumiaji kupata taarifa ya maendeleo ya maombi yao.

Tovuti Kuu ya Takwimu Huria

Wakala imetengeneza Tovuti Kuu ya Takwimu Huria www. opendata.go.tz inayotumika kama dirisha moja la kutolea takwimu huria mbalimbali za Serikali ili kusaidia wananchi na wadau wengine kupata taarifa na takwimu za uendeshaji wa Serikali kwa urahisi na kuzitumia katika  jitihada  za  maendeleo  kiuchumi  na kijamii. Sekta ya Elimu, Afya na Maji zilizopewa kipaumbele katika Mpango wa Pili wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (OGP) wa mwaka 2014/16 zimeweka takwimu katika tovuti hiyo ili kuwezesha umma kuzitumia katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Maudhui ya Tovuti hii yanasimamiwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) pamoja na Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa. Aidha, Wakala ya Serikali Mtandao inasimamia masuala ya kiufundi ya tovuti hii.