Tunafanya nini
Tunafanya nini
Ili kutimiza Dira na Dhamira yake, Wakala ya Serikali Mtandao ina malengo sita, ambayo yakitimizwa yataiwezesha kutimiza masharti ya huduma ya wadau na wateja wake. Malengo hayo ni:-
Kuboresha uwezo wa Taasisi za Serikali kutekeleza jitihada za Serikali Mtandao;
Wakala inaendesha mafunzo mbalimbali ya usimamizi wa mtandao, Mfumo wa Baruapepe Serikalini , Utoaji wa huduma mtandao kwa umma, Ofisi Mtandao, e-vibali na usimamizi wa tovuti kwa taasisi. Pia, Wakala inazishauri na kuzisaidia taasisi mbalimbali za umma kujenga uwezo wa watumishi wake katika kutekeleza jitihada za Serikali Mtandao.
Kuboresha upataji wa huduma mtandao kwa umma;
Wakala ya Serikali Mtandao inaimarisha miundombinu ya msingi kwa ajili ya utoaji wa huduma mtandao kwa umma na kwa wakati, uwazi, urahisi na gharama nafuu. Wakala imetengeneza mifumo ifuatayo; Tovuti Kuu ya Serikali (www.tanzania.go.tz) ambayo ni dirisha moja la kutolea huduma kwa umma, Tovuti Kuu ya Ajira (http://portal.ajira.go.tz/) ambayo inatoa taarifa kuhusu nafasi zote za kazi zinazotangazwa Serikalini, Tovuti za taasisi za umma , Mfumo wa kuhifadhi taarifa za Bunge (http://parliament.go.tz/polis/), Mfumo wa huduma za Serikali kupitia simu za Mkononi *152*00# na Mfumo wa kurusha matukio ya Serikali Mubashara
Kuboresha mifumo shirikishi ya TEHAMA
Wakala inaweka mazingira yanayowezesha taasisi za umma kushirikiana katika matumizi ya rasilimali za TEHAMA ili kuondoa urudufu, kupunguza gharama na kuongeza ubora wa huduma kwa umma kwa kufanya yafuatayo; Imesanifu ujenzi wa kituo kidogo cha kuhifadhi na kuendesha mifumo mbalimbali ya Serikali mtandao, imetengeneza mfumo wa baruapepe wa Serikali, menaunganisha taasisi za umma 149 katika mtandao mmoja wa mawasiliano,inasimamia masafa ya intaneti Serikalini, imetengeneza Mfumo wa Huduma za Serikali Kupitia Simu za Mkononi (mGov) pamoja na Mfumo wa Ofisi mtandao.
Kuimarisha uratibu, usimamizi na uzingatiaji wa viwango vya Serikali Mtandao katika utoaji wa huduma kwa umma;
Wakala imetengeneza Miongozo na Viwango vya Serikali Mtandao vinavyopatikana kwenye tovuti ya Wakala www.ega.go.tz na pia imetengeneza na inaendesha Mfumo wa Maelezo ya Miradi ya TEHAMA Serikalini unaopatikana kupitia https://gip.ega.go.tz.
Kuboresha huduma za ushauri wa kitaalam;
Wakala ya Serikali Mtandao inatoa huduma za ushauri wa kitalaamu na msaada wa kiufundi kwa taasisi za umma. Miongoni mwa misaada hiyo ni kusanifu, kutengeneza na kuendesha Mifumo na tovuti. Pia, imetoa ushauri wa kitaalam katika maeneo ya uhakiki wa Mifumo ya TEHAMA, Tathmini ya Usalama, Utayarishaji wa Mpango wa Kukabili Majanga, Utayarishaji wa Sera ya TEHAMA, Utayarishaji wa Mkakati wa TEHAMA na Usanifu na Tathmini ya Miradi ya TEHAMA.