emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

Serikali kutoa huduma kwa njia ya simu


Serikali kutoa huduma kwa njia ya simu


Serikali inaandaa mazingira bora ya kutoa huduma kwa kutumia simu za mkononi ili kumrahisishia mwananchi kupata huduma za Serikali mahali popote, wakati wowote na kwa haraka zaidi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti wa Huduma za Serikali Mtandao Bw. Michael Moshiro wakati wa mahojiano katika kipindi cha Uchumi Leo kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) Agosti 3, 2016.

“Kwa takwimu za hivi karibu, Tanzania ina zaidi ya watu millioni thelathini ambao wanatumia simu za mkononi, hivyo hatunabudi kama Wakala ya Serikali Mtandao kuziwezesha taasisi za umma kutoa huduma hizo kwa wananchi kwa njia ya Simu za Mkononi” alisema Bw. Moshiro.

Aliongeza kuwa huduma hizi zitawasaidia wananchi kuepuka foleni ambayo inawafanya kupoteza muda mwingi barabarani wakielekea katika ofisi za umma kutafuta huduma ambazo wangeweza kuzipata kwa njia ya Mtandao au simu za mkononi.

“Chukua mfano, wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Oktoba 2015, wananchi waliwezeshwa kwa njia ya simu kuangalia kama kitambulisho cha kupigia kura ni sahihi na atapigia eneo gani. Huduma hii ililenga kumrahisishia mwananchi kupata taarifa mahali alipo. Hivyo, kumfanya aendelea na shughuli za kujenga uchumi wa nchi”. Aliongeza Bw. Moshiro

Vile vile aliongeza kuwa, kupitia Tovuti Kuu ya Serikali inayopatika kwa anuani ya www.tanzania.go.tz yenye taarifa mbalimbali za Serikali, inawawezesha wawekezaji kuona fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo hapa nchini na hivyo kuwekeza na kukuza uchumi.

Aidha, alisisitiza kuwa huduma mtandao zitasaidia kuondoa urasmu, mianya ya rushwa, kuharakisha utoaji maamuzi na hatimaye kuwavutia wawekezaji walio wengi na kukuza uchumi wa Taifa.