Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Wakala ya Serikali Mtandao.

Rasilimali Shirikishi

Rasilimali Shirikishi

Rasilimali za TEHAMA Serikalini zilikuwa zimetawanyika na hivyo kila taasisi ya umma ilikuwa inapanga na kutekeleza jitihada zake yenyewe. Hii ilisababishwa na kutumika kwa viwango tofauti vya serikali mtandao vilivyosababisha urudufu wa mifumo, kuwa na mifumo isiyowasiliana na gharama kubwa za uendeshaji wa jitihada za TEHAMA. Wakala iliweka mazingira ya utekelezaji wa serikali mtandao kwa ufanisi na kwa uwiano zaidi kwa kuanzisha miundombinu shirikishi ya serikali mtandao kama vile Mtandao wa Mawasiliano Serikalini – GovNet, Kituo cha Kuhifadhi Mifumo na Data – GDC, Mfumo Huduma za Simu za Mkononi -mGov, na Mifumo Shirikishi (Mfumo wa Baruapepe Serikalini– GMS na Mfumo wa Ofisi Mtandao – GeOS. Vilevile Wakala ilitoa msaada wa kiufundi na ushauri katika utengenezaji na utekelezaji wa mifumo shirikishi kama vile Tovuti ya Taifa ya Biashara, Ununuzi Mtandao na uendeshaji wa mifumo shirikishi iliyopo.

Mtandao wa Mawasiliano ya Serikali (GovNet)

Wakala imeanzisha Mtandao wa mawasiliano wa Serikali ambao ni shirikishi, ulio salama na wa gharama nafuu. Hadi sasa Wizara, Idara na Wakala 72 na Mamlaka za Serikali za Mitaa 77 zimeunganishwa kwenye mtandao huo. Baadhi ya Wizara, Idara Zinazojitegemea na Wakala za Serikali ni: Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya Afya, Wizara ya Mambo ya Nje na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Mambo ya Ndani ambazo tayari zimehamia Dodoma na zimeunganishwa kwenye mfumo wa mawasiliano ya Serikali.

Mamlaka za Serikali za Mitaa 77 katika mikoa 20 ya Tanzania Bara imeunganishwa. Aidha, vituo mablimbali vimeunganishwa ikiwa ni pamoja na hospitali za mikoa, Ofisi za Sekretarieti za Mikoa, Halmashauri za Wilaya na Manispaa au Jiji. Pia Kituo cha Uendeshaji Mtandao (NOC) kimeanzishwa kwa dhumuni la ufuatiliaji wa mtandao, utoaji taarifa wa matatizo na kushughulikia matukio wakati wote (24/7). Mtandao wa Serikali na Kituo cha Intaneti (TIX) vimeunganishwa katika kiungo cha 1 Gbps chenye wastani wa matumizi ya 0.85 inayoboresha upatikanaji wa huduma kwa watoa huduma nchini.

Kituo cha Kuhifadhi Mifumo na Data (GDC)

Serikali imejenga vituo vya kisasa vya kuhifadhi mifumo na data ili kuboresha mazingira ya kuhifadhi rasilimali shirikishi miongoni mwa taasisi za umma. Vituo hivyo vinatoa huduma za uhifadhi wa awali, mahali mbadala (co-location), kujikinga na majanga kwenye mitandao na mifumo tumizi na usajili wa vikoa na majina miliki ya tovuti (.go.tz).

Usimamizi wa Masafa ya Intaneti Serikalini 

Serikali imenunua haki miliki za kutumia masafa ya intaneti (IRU) kiasi cha 1.55 Gbps yanayowasilishwa serikalini kupitia mkongo wa baharini kwa watoa huduma wa SEACOM na EASSY. Kuanzia mwaka 2012 hadi sasa Wakala kama msimamizi wa masafa hayo imepokea na kuidhinisha maombi 182 ya taasisi za umma ikiwemo hospitali za umma, shule na vyuo vikuu.

Mfumo wa Huduma za Serikali Kupitia Simu za Mkononi (mGov)

Mfumo wa Huduma za Serikali Kupitia Simu za Mkononi (mGov) http://mgov.ega.go.tz ulitengenezwa mwaka 2015 kwa lengo la kujumuisha huduma zote za simu za mkononi Serikalini. Mfumo huu unatumia arafa (sms) katika kutoa na kupokea taarifa. Taarifa hizi zinaweza kutoka Serikalini kwenda kwa wananchi au kutoka kwa wananchi kwenda serikalini kupitia namba 15200. Pia inatoa menyu ya namba za huduma za serikali (USSD) *152*00#. mGOV imeunganishwa na watoa huduma wa simu za mkononi nchini Tanzania na jumla ya taasisi za umma 117 zinatumia huduma hiyo na miamala zaidi ya milioni 15 imefanyika.

Mfumo wa Baruapepe Serikalini (GMS)

Wakala imesanifu, imetengeneza na inaendesha Mfumo wa Baruapepe Serikalini (GMS) baada ya kufanya uchunguzi makini wa mifumo iliyokuwa ikitumiwa na taasisi za umma katika mawasiliano na kubainika kuwa mawasiliano ya baruapepe yanakabiliwa na changamoto mbalimbali za mtawanyiko, usalama na kutoaminika. Kwa sasa jumla ya taasisi za umma 359 zikiwemo ofisi za balozi zetu zinatumia mfumo huu. 

Mfumo wa Ofisi Mtandao (GeOS)

Mfumo wa Ofisi Mtandao (GeOS) ulitengenezwa ili kuwezesha na kurahisisha shughuli za utawala ndani ya Serikali. Shughuli hizo zinahusu mzunguko wa mafaili na nyaraka ndani na miongoni mwa taasisi za umma. Mfumo huu unapatikana kupitia https:// eoffice.gov.go.tz kwa taasisi zote za umma zilizounganishwa kwenye Mtandao wa Mawasiliano Serikalini (GovNet) kwa kutumia anuani rasmi ya baruapepe ya serikali. Hadi kipindi cha taarifa hii jumla ya taasisi za umma 28 zimewezeshwa kutumia mfumo huu.