Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Wakala ya Serikali Mtandao.

Udhibiti wa Viwango

Udhibiti wa Viwango

Utekelezaji wa Serikali Mtandao unategemea kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa Sera, Sheria, Kanuni, Miongozo na Viwango. Awali, kulikuwepo na Sera ya TEHAMA ya mwaka 2003, Waraka wa Utumishi Na.5 wa mwaka 2009 kuhusu Matumizi Bora na Salama ya Vifaa na Mifumo ya TEHAMA, Waraka wa Utumishi Na.6 wa mwaka 2009 unaohusu Utunzaji na Utekelezaji wa Taarifa zilizo kwenye Mfumo wa kielektroni, Sheria ya Mawasiliano ya Kimtandao na Posta, 2010 pamoja na Mwongozo wa Matumizi Bora, Sahihi na Salama ya Vifaa na Mifumo ya TEHAMA Serikalini, 2012 ambazo hazikutosheleza utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao. Hali hiyo ilisababisha mifumo michache iliyokuwepo kutowasiliana na kutofautiana viwango na ufanisi. Vilevile, kulikuwa na kiwango kidogo cha matumizi ya TEHAMA miongoni mwa Taasisi za Umma katika utoaji huduma kwa umma.

 Serikali imetekeleza jitihada mbalimbali za Serikali Mtandao zikiwemo kupitia na kutoa Sera mpya ya TEHAMA 2016, kutunga Sheria ya Miamala ya Mtandaoni 2014 na kutunga Sheria ya Makosa ya Kimtandao ya mwaka 2015. Hivi karibuni Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Wakala imetengeneza Miongozo na Viwango vya Serikali Mtandao vinavyopatikana kwenye tovuti ya Wakala www.ega.go.tz kwa matumizi ya Taasisi za Umma katika kusanifu, kutengeneza na kuendesha mifumo na miundombinu ya TEHAMA kulingana na mahitaji ya shughuli zao.

Miongozo na viwango hivyo vimegawanywa katika makundi tisa ambayo ni Usanifishaji Programu Tumizi za Serikali Mtandao, Usanifishaji Shughuli za Serikali Mtandao, Usanifishaji wa Taarifa za Serikali Mtandao, Usanifishaji wa Miundombinu ya Serikali Mtandao, Mfumo wa Serikali Mtandao Kuwasiliana, Usanifishaji wa Usalama wa Serikali Mtandao, Usanifishaji wa Dira ya Serikali Mtandao, Usanifishaji Utangamanishi wa Serikali Mtandao na Mchakato wa Serikali Mtandao na Usimamizi. 

Wakala inasimamia uzingatiaji wa viwango, miongozo na taratibu za Serikali Mtandao. Katika kusimamia uzingatiaji wa kanuni na sheria, Wakala pamoja na mambo mengine imetengeneza na inaendesha Mfumo wa Maelezo ya Miradi ya TEHAMA Serikalini unaopatikana kupitia https://gip. ega.go.tz wa mwaka 2015 ili kusimamia na kudhibiti miradi ya TEHAMA Serikalini.