Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Wakala ya Serikali Mtandao.

Huduma Mtandao

Huduma Mtandao

Kabla ya mwaka 2012, kulikuwa na njia chache za kutolea huduma mtandao kwa umma. Njia hizo ni pamoja na tovuti za Serikali ambazo hata hivyo zilizotoa taarifa tu, zilisimamiwa na wakandarasi, maudhui hayakuhuishwa mara kwa mara na kutopatikana kwa urahisi. Katika kipindi cha miaka mitano, Wakala imetengeneza na kuboresha miundombinu na mifumo inayowezesha upatikanaji wa huduma kwa umma. Baadhi ya jitihada hizo ni:

Kuhuisha na Kusanifu Upya Tovuti ya Serikali kuwa Tovuti Kuu

Mwaka 2012, Wakala ilihuisha Tovuti ya Serikali na kuifanya kuwa Tovuti Kuu (www.tanzania.go.tz) ambayo ni kituo kimoja cha upatikanaji wa taarifa na huduma za Taasisi za Umma. Maudhui ya tovuti hii yapo katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza na yamegawanywa kwenye sehemu saba ambazo ni: Taifa Letu, Wananchi, Serikali, Biashara, Mambo ya Nje, Nifanyeje na Matangazo. 

Tovuti hii inasimamiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Kwa mujibu wa uchambuzi wa Google kwa mwezi Desemba 2017, nchi 172 zimetembelea tovuti hiyo kwa maudhui mbalimbali hasa Nyaraka, Mpangilio Orodha, Fomu, Nifanyeje na Matangazo. Kwa kutembelea sehemu ya huduma za simu za mkononi na huduma mtandao kwenye tovuti unaweza kupata huduma mtandao zinazotolewa na Taasisi za Umma.

Tovuti za Taasisi za Umma 

Wakala imesanifu na kutengeneza tovuti 411 kwa taasisi za umma ambapo tovuti 200 ni za Wizara, Idara Zinazojitegemea na Wakala, 26 za Sekretarieti za Mikoa na 185 za Mamlaka za Serikali za Mitaa. Lengo ni kuwezesha utoaji na upatikanaji wa taarifa kwa umma kwa urashisi na kwa gharama nafuu. Maudhui katika tovuti hizo husimamiwa na taasisi husika.

Tovuti Kuu ya Ajira (http://portal.ajira.go.tz)

Tovuti Kuu ya Ajira imesanifiwa na kutengenezwa mwaka 2013 na inasimamiwa na Sekretarieti ya Ajira iliyopo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Tovuti hii ni mfumo unaowezesha baadhi ya michakato ya ajira iliyokuwa ikifanywa kwa mkono kufanyika kielektroni. Hadi Desemba 2017, tovuti hiyo ilikuwa na watumiaji waliojisajili 221,081 ambao 164,513 walikuwa amilifu na 56,568 si amilifu na jumla ya maombi ya kazi 427,428 yametumwa kupitia tovuti hii.

Mfumo wa Kuhifadhi Taarifa za Bunge (http://parliament.go.tz/polis/) 

Mfumo huu unatumika kuhifadhi taarifa mbalimbali za Bunge kama vile miswada na sheria, hotuba, kumbukumbu za vikaovinavyofanyika katika vipindi vya Bunge, kanzi data ya Waheshimiwa Wabunge na majimbo wanayowakilisha. Mfumo huu unasimamiwa na kuratibiwa na Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Huduma za Serikali Kupitia Simu za Mkononi

Wakala imeziwezesha taasisi za umma kutoa huduma mtandao kupitia teknolojia ya simu za mkononi kwa kuzipatia namba ya arafa na/au USSD ili kuwezesha na kurahisisha malipo ya huduma mbalimbali kwa mfano leseni za udereva, faini za makosa ya barabarani, uhakiki wa wateja wa NHIF na utoaji taarifa za rushwa kwa PCCB. 

Mfumo wa Kurusha matukio ya Serikali Mbashara 

Wakala imebunina kutengeneza mfumo unaowezesha kurushwa mbashara matukio muhimu ya Serikali kwa njia ya mtandao kupitia tovuti Kuu na na tovuti ya taasisi husika inapohitajika. Baadhi ya taasisi zinazotumia huduma hiyo ni Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Bunge na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kutangaza matokeo ya nafasi ya Urais katika Uchaguzi Mkuu. Aidha, huduma hii hutolewa na Wakala kwa kushirikiana na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).