emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

e-GA YATOA VIFAA TIBA KWA WAJAWAZITO


e-GA YATOA VIFAA TIBA KWA WAJAWAZITO


Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani mwaka 2025, Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imetoa msaada wa vifaa tiba na mahitaji muhimu kwa wajawazito na akina mama waliojifungua, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma (General) na Hospitali ya Mbagala ya jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Meneja Mawasiliano wa e-GA Bi. Subira Kaswaga alisema, e-GA inatambua umuhimu wa kumuwezesha mwanamke mwenye uhitaji ili kujenga taifa bora.

Bi. Subira aliongeza kwamba, msaada huo ni moja ya njia inayoonesha namna ambavyo Mamlaka hiyo inavyomthamini mwanamke.

Alisema katika kuhakikisha jamii inapata huduma bora za afya, e-GA imekuwa ikishirikiana na Wizara ya Afya kutengeneza mifumo mbalimbali ya TEHAMA inayorahisisha utoaji wa huduma za afya kwa jamii wakiwemo wanawake na watoto.

“Tunatambua kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza katika sekta ya afya kwa kujenga vituo vya afya pamoja na kuboresha miundombinu yake, nasi e-GA tunaunga mkono jitihada za Serikali kwa kutengeneza mifumo ya TEHAMA, inayorahisisha utendaji kati katika sekta ya afya ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za afya kwa urahisi zaidi,” alisema Bi. Subira.

Aliongeza kuwa, mifumo ya TEHAMA huimarisha haki na usawa katika utoaji wa huduma za Serikali, bila kujali jinsia au hali ya kiuchumi na kutoa nafasi sawa kwa wote katika kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi na kielimu zinazopatikana katika TEHAMA.

“Kama isemavyo kauli mbiu ya mwaka huu juu ya haki usawa na uwezeshaji kwa wanawake, e-GA kupitia Kituo cha Utafiti na Ubunifu wa Serikali Mtandao hutoa nafasi kwa wanafunzi wa TEHAMA wa vyuo vikuu, kushiriki mafunzo kwa vitendo na mafunzo kazini, hii ni namna moja wapo inayoonesha jinsi gani e-GA tunaishi katika kauli hii ya kuimarisha usawa na haki kwa jinsia zote,” alisisitiza Bi. Subira.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma, Bi. Tegemea Ngulwa, na Dkt Ally Mussa Mganga Mfawidhi Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu, waliishukuru e-GA kwa msaada huo na kuomba kuendeleza ushirikiano katika kuwasaidia wagonjwa wenye uhitaji katika hospitali hizo.