emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

e-UKAGUZI: KUONGEZA UFANISI KATIKA SEKTA YA UKAGUZI NCHINI


e-UKAGUZI: KUONGEZA UFANISI KATIKA SEKTA YA UKAGUZI NCHINI


Utekelezaji wa Jitihada za Serikali Mtandao, unategemea uwepo wa mfumo imara wa ukaguzi utakaoboresha na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika kaguzi mbalimbali zinazofanywa na wakaguzi ndani na nje ya Taasisi za Umma.

Mfumo mpya wa kaguzi ujulikanao kama e-Ukaguzi ni mfumo unaosaidia na kuimarisha utendaji kazi wa kaguzi za ndani za Taasisi za Umma, ikiwemo kuandaa mpango kazi wa mwaka, kutekeleza kaguzi, kufanya ufuatiliaji wa hoja mbalimbali za kikaguzi ndani na nje ya taasisi, pamoja na kufanya uchambuzi wa vihatarishi vikubwa katika maeneo yote ya taasisi yanayokaguliwa.

Mfumo huu jumuishi ni matokeo ya ubunifu uliofanywa na wazawa kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) katika kuhakikisha kuwa matumizi ya TEHAMA Serikalini yanaimairishwa na huduma mbalimbali zitolewazo kwa Wananchi zinaboreshwa.

Meneja wa Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGovRIDC) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao Dkt. Jaha Mvulla, amesema kuwa, lengo la kuanzishwa kwa mfumo huu ni kurahisisha utendaji kazi kwa wakaguzi wa ndani, kupunguza matumizi ya karatasi, kuongeza ufanisi na kupunguza muda wa kufanya kaguzi mbalimbali.

Amefafanua kuwa, mfumo huo unaruhusu wakaguzi wa ndani kupanga, kutekeleza na kufuatilia matokeo ya kaguzi, unachakata na kurahisisha upatikanaji wa ripoti mbalimbali kama vile ripoti za mwaka, mwezi na kuwapa uwezo Wakuu wa Idara kujibu kila hoja zitokanazo na kaguzi zote zinazohusu Idara zao.

“Mfumo unatoa nafasi kwa Wakaguzi wa Ndani kuweka na kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa hoja za kaguzi za nje ya taasisi kama zile za CAG, PPRA, OSHA, BOT na nyinginezo zinazohusu utendaji wa taasisi hizo”, amesema Dkt. Jaha.

Ameongeza kuwa, e-GA imesanifu mfumo huo kutokana na uhitaji mkubwa wa kuboresha na kuongeza ufanisi wa kazi mbalimbali za kaguzi za Taasisi za Umma wakati wa kuandaa mpango kazi, ili kuhakikisha kuwa kaguzi zote zinazofanyika zinakuwa na tija kwa taasisi na kuwa, mfumo huo kwa sasa upo katika hatua ya majaribio kwenye taasisi mbalimbali za umma.