Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imemtangaza Afisa TEHAMA Bw. Obed Makombe kuwa mfanyakazi bora wa Mamlaka kwa mwaka wa fedha 2024/2025 huku uwajibikaji na weledi vikitajwa kuwa msingi mkuu wa ushindi huo.
Uchaguzi wa mfanyakazi bora wa Mamlaka ulifanyika Februari 26, mwaka huu, baada ya kuwashindanisha wafanyakazi bora 10 kutoka katika idara na vitengo, na kisha Menejimenti kupiga kura ili kumpata mfanyakazi bora wa Mamlaka kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mhandisi. Benedict Ndomba amesema, zoezi la uchaguzi wa mfanyakazi bora hulenga kuchochea utendaji kazi wenye kuzingatia uadilifu na weledi kwa maslahi mapana ya Taifa.
Mhandisi. Ndomba alisema kuwa, e-GA inatambua na kuthamini mchango wa watumishi wake wote katika kufikia malengo ya taasisi na kuwa, uchaguzi wa mfanyakazi bora ni motisha kwa wafanyakazi wote kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi na weledi huku wakizingatia misingi mikuu ya Mamlaka.
“Mamlaka inatambua na kuthamini mchango wa watumishi wote katika kufanikisha malengo ya Taasisi, hivyo nitoe rai kwa watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu lakini pia niwapongeze sana watumishi bora waliochanguliwa kwa mwaka huu wa 2024/2025,” alisema Ndomba.
Alibainisha kuwa, Mamlaka itaendelea kuboresha na kuimarisha mazingira ya kazi ikiwemo, kutoa vitendea kazi kwa wakati, chakula na mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi wake ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
Naye, Meneja Rasilimaliwatu na Utawala Bw. Erick Kalembo alisema, Mamlaka ilifanya uchaguzi wa ndani kwa kila Idara na vitengo ili kupata mfanyakazi bora na kisha orodha hiyo iliwasilishwa Menejimenti kwa ajili ya kumchagua mfanyakazi bora wa taasisi.
Alisema, Menejimenti iliwapima watumishi wote bora waliochaguliwa kutoka kwenye Idara na Vitengo na kisha kupiga kura kwa uwazi ili kumchagua mfanyakazi bora wa Mamlaka, kwa kuzingatia vigezo vilivyopo bila upendeleo wa aina yeyote.
Uchaguzi huo ulifanyika kwa kupiga kura na kuwapata washindi watatu walioingia tatu bora na hatimaye kumpata mfanyakazi bora wa jumla wa Taasisi.
“Tuliangalia vigezo mbalimbali vya mfanyakazi bora ikiwemo nidhamu, uadilifu na utekelezaji wa majukumu ya mtumishi kupitia mfumo wa upimaji kwa watumishi wa e-SS”, alisema Bw. Kalembo.
Naye Mfanyakazi bora wa Mamlaka Bw. Obed Makombe, ametoa shukrani zake kwa watumishi na menejimenti ya Mamlaka kwa kutambua juhudi na utendaji kazi wake, uliopelekea kuchagulia kupata ushindi huo.
“Napenda kuwashukuru watumishi wenzangu kwa kutambua utendaji kazi wangu lakini pia nawashukuru kwa ushirikiano wao kwani katika taasisi hata ukiwa mfanyakazi bora ni lazima ushirikiane na wafanyakazi wengine ili kufikia malengo ya taasisi, naahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi zaidi”, alisema Bw. Obed.
Nafasi ya pili imeshikwa na Bw. Melkizedeck Ndabayoye King'ani (Afisa Tawala Mwandamizi) kutoka Idara ya Huduma za Uwezeshaji na nafasi ya tatu kushikwa na Bw. Kulwa Gibaka (Muhasibu) kutoka Idara ya Uhasibu na Fedha.