emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

TEHAMA INACHOCHEA MABADILIKO YA KWELI KWA VIJANA: FRANK ALEX


TEHAMA INACHOCHEA MABADILIKO YA KWELI KWA VIJANA: FRANK ALEX


Ari ya vijana katika kuifahamu na kutumia fursa zilizopo katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), imekuwa ni kichocheo katika kuleta mapinduzi ya kiteknolojia nchini.

Hii inatokana na ukweli kuwa, TEHAMA inazidi kukua kila uchwao na kuvutia vijana wengi kutokana na fursa mbalimbali zinazopatikana zikiwemo za kielimu na kiuchumi.

Kutokana na uwepo wa fursa hizo, vijana wengi hupenda kutumia TEHAMA ili waweze kutimiza ndoto zao za kielimu, kiuchumi sambamba na kuleta mabadiliko chanya katika jamii kupitia TEHAMA.

Frank Alex, ni muhitimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) katika Shahada ya Uhandisi wa Kompyuta ‘Bachelor of Science in Computer Engineering’ ambaye kwa sasa, anajitolea katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GOVRIDC) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).

Alianza kupenda masomo ya TEHAMA, pale alipoamua kujiunga na klabu ya kompyuta alipokuwa shule ya Sekondari ya Benjamin William Mkapa iliyopo jijini Dar-es-Salaam.

Kujiunga kwake katika Klabu hiyo, ndiyo ulikuwa mwanzo wa safari yake ya kutaka kuleta mageuzi ya TEHAMA nchini, na kuwa miongoni mwa kundi la vijana wanaoamini katika matumizi sahihi ya TEHAMA, ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii yakiwemo ya kielimu, afya, kiuchumi n.k.

“TEHAMA hutumika kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii yetu, na kwa msingi huo sisi vijana tunaamini kuwa tukijiendeleza katika fani hii kwa ufanisi mzuri, tunaweza kuchangia mageuzi ya kitaifa katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu, uchumi na nyinginezo.”, anasema Bw. Frank.

Anabainisha kuwa, mapenzi yake katika TEHAMA hayakuja kwa bahati mbaya, bali uwepo wa sababu nyingi zilizomfanya awe na hamu ya kujifunza na kujitosa katika uwanja huu.

Shauku yake kubwa ilikuwa ni kujua jinsi mambo yanavyofanya kazi, jinsi kompyuta na teknolojia nyingine zinavyotengenezwa na kama hiyo haitoshi, ni pale alipowaona vijana wenzake wakipata mafanikio makubwa kupitia TEHAMA na hivyo kumuongezea shauku ya kutaka kujifunza zaidi.

“Niliona vijana walionitangulia wakitengeneza tovuti, programu za simu, au hata kujiunga na fursa za kujiajiri kupitia intaneti (mtandao), na hili lilinifanya niwe na nia ya kutaka kufanikiwa kama wao”, anafafanua Bw. Frank.

Mtaalamu huyu chipukizi anasema, mapenzi na TEHAMA yaliongezeka zaidi baada ya kugundua kwamba TEHAMA ni chanzo cha fursa nyingi za ajira serikalini na sekta binafsi na hata kujiajiri mtu binafsi.

Anataja baadhi ya njia zinazotumiwa na vijana kujiajiri ni pamoja na kutumia mitandao maarufu ya ‘Upwork’ na ‘Fiverr’, ambayo imekuwa ni majukwaa muhimu kwa vijana kuonesha uwezo wao na kupata ajira zinazowapa uhuru wa kiuchumi.

Anabainisha kuwa, kwa sasa vijana wengi wanaweza kujiendeleza na kujiongezea ujuzi katika TEHAMA, kutokana na uwepo wa majukwaa mengi kama vile ‘Coursera’ na ‘Udemy’, ambayo yanatoa njia ya kupata elimu bora kwa gharama nafuu, na kuhimiza vijana wengi kutumia fursa hiyo kujiendeleza katika teknolojia ili kukuza utaalamu wao.

Frank anasema kuwa, TEHAMA ina nafasi kubwa katika kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii zetu, ikiwemo kutumia Teknolojia ya ‘Internet of Things’ (IoT), inayotoa suluhu kwa masuala ya nishati mbadala, ambapo zinaweza kutengeneza bunifu zinazohusiana na uzalishaji wa nishati au vifaa vya ki-electroniki kwa matumizi ya ndani.

“Bunifu hizi pia zitakuwa ni suluhisho la kupunguza utegemezi kwa nchi za nje na kuongeza uwezo wetu katika sekta za viwanda na uzalishaji,” anasisitiza Bw. Frank.

Aidha, anabainisha kwamba mifumo ya teknolojia kama Akili Mnemba (AI) na Machine Learning (ML), zimekuwa na mchango mkubwa katika kubuni suluhu katika sekta za afya na kilimo.

Bw. Alex anasema, katika miaka ya hivi karibuni TEHAMA imetoa fursa kwa vijana wa Tanzania kujiingizia kipato kwa kufanya biashara kupitia mitandao ya kijamii kama Instagram, WhatsApp, na tovuti zao binafsi, na hivyo kuongeza kipato chao na kusaidia uchumi wa nchi.

“Uwepo wa majukwaa kama ‘YouTube’, ‘podcaster’ na utengenezaji wa aplikesheni tumizi, umeongeza wigo wa fursa kwa vijana kuonyesha ubunifu wao na kujiajiri kupitia njia za kidijitali, hii ni faida kubwa kwa taifa, kwani inasaidia kupunguza tatizo la ajira na kuongeza kiwango cha ushiriki wa vijana katika kujenga uchumi wa nchi kidijitali.” anafafanua.

Aidha, Bw. Alex ameishauri Serikali kuendelea kuwekeza katika elimu ya TEHAMA kuanzia ngazi ya msingi, sekondari hadi Vyuo Vikuu, ili kuhakikisha vijana wengi wanapata ujuzi wa kimsingi wa fani hiyo wakiwa katika umri mdogo.

Anasisitiza kuwa, ni vema Serikali ikaanzisha na kuendeleza vituo vya tafiti na ubunifu (Research and Innovation Centers) katika vyuo vikuu na shule za sekondari, ili kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha ubunifu wa vijana na kuwawezesha kutafuta suluhisho la matatizo ya kijamii kupitia TEHAMA.

Frank anaamini kuwa, uwepo wa vituo hivyo utasaidia vijana wengi kukuza vipaji vyao katika TEHAMA, kwa kutengeneza mifumo na bunifu zinazoweza kutatua changamoto mbalimbali za kiuchumi, afya, kilimo na kijamii.