emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

WATUMISHI WAASWA KULINDA AFYA ZAO


WATUMISHI WAASWA KULINDA AFYA ZAO


Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), wametakiwa kulinda na kuimarisha afya zao kwa kufanya mazoezi mara kwa mara, ili kuepukana na hatari ya kupata magonjwa sugu yasiyoambukizwa.

Hayo yalisemwa na Dkt. Hafidh Ameir, Afisa anayeratibu Afua za VVU mahali pa kazi ngazi ya taifa, katika sekta ya umma kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Februari 27 mwaka huu, wakati wa kikao cha mwaka cha watumishi jijini Dar Es Salaam.

Alibainisha kuwa, asilimia kubwa ya watumishi wa umma wapo katika hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo ugonjwa wa shinikizo la damu na kisukari, hali inayosababishwa na kutokuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi mara kwa mara pamoja na ulaji wa vyakula usiozingatia lishe bora.

“Ili tuweze kujilinda dhidi ya magonjwa haya, ni lazima tujenge utaratibu wa kufanya mazoezi mepesi ya kutembea kwa dakika chache kila baada ya saa moja tunapokuwa kazini, ili kuruhusu damu kuzunguka mwilini, kwani tunatumia muda mwingi kukaa bila kuinuka,” alisema Dkt. Ameir.

Aliongeza kuwa, ni vizuri kuzingatia mlo kamili na kujiepusha na vyakula vya viwandani ambavyo huchangia kwa kasi uwezekano wa kupata magonjwa sugu yasiyoambukiza.

Naye Daktari wa Magonjwa ya Saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt. Maguha Stephano, aliwahimiza watumishi kujenga utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara ili kubaini dalili za awali za ugonjwa wa saratani.

Alisema kuwa, utaratibu wa kupima afya mara kwa mara ni muhimu kwani huwezesha kubaini hatua za awali za ugonjwa wa saratani na hivyo kuweza kutibika mapema, na ikiwa dalili zitaonekana katika hatua za mwisho huwa na uwezakano mdogo wa kupona kwa mgonjwa.

“Changamoto tuliyonayo ni wagonjwa kuja hospitalini kwa kuchelewa wakiwa wameshazidiwa unakuta ule ugonjwa tayari umeshakomaa na hautibiki tena, lakini kama mgonjwa huyu angewahi mapema ageweza kupona,” alisisitiza Dk. Maguha.

Aliongeza kuwa, utaratibu wa kupima afya mara kwa mara si kwa ajili ya kuangalia VVU peke yake bali hata kwa magonjwa yasiyoambukiza kama vile saratani, na wakati mwingine inaweza kuwa ya kurithi hivyo tahadhari zikachukuliwa mapema.

Aidha, Mtaalamu wa afya ya akili kutoka Taasisi ya Afyachek Dkt. Isaac Maro, aliwataka watumishi wa Mamlaka kutunza afya ya akili ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza baadaye.

Alisema, afya ya akili ni muhimu kwa ustawi wa mwanadamu, hivyo ni lazima watu wote wajifunze kuweka usawa wa maisha kwa kutenga muda wa kazi, muda binafsi na muda unaohitaji kushiriki mambo mbalimbali ya kijamii.

“Watu wengi wanapata changamoto ya afya ya akili kwa kuwa na msongo mkubwa wa mawazo na kushindwa kuweka usawa katika maisha ya kila siku, muda wa kazi utumike kazini na muda binafsi utumike kwa mambo binafsi”, alisema Dkt. Maro.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa watu kuzungumza na watu wakaribu yao au wataalam wa saikolojia wanapopata changamoto za kimaisha ili kupata ushauri sahihi na kwa wakati na kuepukana na kufanya maamuzi yasiyo sahihi ikiwemo kujiingiza katika ulevi wa kupindukia au kujiua.