emblem
Mamlaka ya Serikali Mtandao
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO/IEC 27001:2022 | ISO 9001: 2015
ega Logo
Habari
ega-svg-tree

Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imefanya ziara ya mafunzo na kubadilishana uzoefu kuhusu uendeshaji wa vituo vya huduma kwa wateja (Call Centers and Customer Support) katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Benki ya CRDB na Kampuni ya DStv. Ziara hiyo ya siku tatu ilifanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 21 hadi 23, 2026.

Akielezea lengo la ziara hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za TEHAMA wa e-GA, Bw. Ricco Boma, alisema Mamlaka ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha kituo chake cha huduma kwa wateja, hivyo iliona umuhimu wa kujifunza mbinu bora kutoka taasisi zilizofanikiwa katika eneo hilo.

“Tumekuja kujifunza namna wanavyosimamia mawasiliano ya wateja, kupokea na kushughulikia malalamiko, teknolojia inayotumika pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali ili kuboresha huduma na kuongeza ufanisi,” alisema Boma.

Aidha, Meneja wa Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao cha e-GA Dkt. Jaha Mvulla, alisema watumishi waliojumuika katika ziara hiyo wamejifunza matumizi ya mifumo ya kisasa ya usimamizi wa huduma kwa wateja, uchambuzi wa takwimu na mbinu za kuhakikisha huduma zinatolewa kwa wakati na kwa ubora unaokidhi matarajio ya wananchi.

Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Uhakiki wa Ubora wa Huduma ‘Senior Manager Service Quality Assurance’ wa Benki ya CRDB, Bw. Anthony Kigoda, aliwahamasisha watumishi wa e-GA kuendelea kujifunza teknolojia na mifumo ya huduma kwa wateja ili wawe mabalozi wazuri katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika utoaji wa huduma kwa wateja.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja wa DStv, Bw. Davis Mihyo, aliipongeza e-GA kwa kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika masuala ya huduma kwa wateja na teknolojia zake.

Aidha, Meneja wa Huduma kwa Wateja TANESCO, Bw. Shamu Lameck Ruteyo, alisema msingi wa huduma bora kwa wateja ni usikivu, mifumo yenye ufanisi na uwezo wa kutatua changamoto za wateja kwa haraka.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa ziara hiyo, Afisa TEHAMA Mwandamizi wa e-GA, Bw. Juvenali Tarimo, alisema mafunzo hayo yataimarisha utoaji wa huduma za Serikali kwa wananchi kupitia matumizi ya teknolojia za kidijitali na kuchochea maboresho ya huduma katika taasisi za umma.

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za e-GA za kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi na kuwajengea uwezo watumishi wake ili kuboresha utoaji wa huduma za Serikali kupitia mifumo ya kidijitali yenye ufanisi na inayozingatia mahitaji ya wananchi.

Mpangilio