emblem
Mamlaka ya Serikali Mtandao
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO/IEC 27001:2022 | ISO 9001: 2015
ega Logo
Habari
ega-svg-tree

Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) imeendelea kuimarisha utafiti na ubunifu wa teknolojia ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI) kupitia Kituo chake cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-Government Research, Innovation and Development Centre -AI), kwa kutengeneza mifumo inayotumia AI ambayo kwa sasa ipo katika hatua ya majaribio (pilot).

Akizungumza hivi karibuni, kuhusu mikakati ya e-GA katika matumizi ya teknolojia mpya ikiwemo AI Meneja Mawasiliano wa e-GA Bi. Subira Kaswaga amesema, e-GA imejipanga kuendana na matumizi ya teknolojia mpya zinazoibukia kwa kufanya tafiti na bunifu mbalimbali za mifumo itakayoweza kutumika ndani ya Serikali, ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Hadi sasa,  mifumo iliyosanifiwa kupitia kituo hiki ni pamoja na Msaada AI, Muhtasari AI na Tafsiri AI.  Mifumo hii inalenga kurahisisha uchambuzi wa nyaraka, upatikanaji wa taarifa kwa haraka na kwa usahihi, pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi", alifafanua Meneja huyo.

Aidha, Subira alibainisha kuwa kwa sasa mfumo wa Msaada AI unatumiwa na taasisi mbili ambazo ni Bodi ya Utalii Tanzania katika tovuti yake na Ofisi ya Rais UTUMISHI katika mfumo wa e-Mrejesho, huku e-GA ikiendelea kupokea maboresho yanayojitokeza kulingana na mahitaji au maoni ya watumiaji wa mifumo hiyo.

Alisema, kupitia Kituo cha Utafiti na Ubunifu, e-GA inaendelea kubuni matumizi ya teknolojia mpya zinazokwenda sambamba na mabadiliko ya kidijitali yanayojitokeza duniani, huku ikihakikisha mifumo inayotengenezwa inakidhi mahitaji ya taasisi za umma na wananchi.

"Kwa sasa tunaendelea kufanya utafiti na kutengeneza mifumo inayotumia Akili Unde. Mifumo hiyo ipo katika hatua za majaribio na inalenga kuboresha utoaji wa huduma za serikali kwa kutumia teknolojia za kisasa," alisema Subira.

Alieleza kuwa, AI inatarajiwa kusaidia katika kutafsiri lugha mbalimbali, ikiwemo lugha za asili na lugha ya alama, ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kupata huduma za serikali bila vikwazo vya lugha au ulemavu wa mawasiliano.

Vilevile, Subira alisema e-GA inaendelea kufanya utafiti wa teknolojia ya uhalisia pepe (Virtual Reality – VR), ambayo humwezesha mtumiaji kutembelea maeneo mbalimbali kwa njia ya mtandao bila kufika eneo husika, pamoja na teknolojia ya ‘Blockchain’ kwa lengo la kuimarisha usalama, uwazi na ufanisi wa mifumo ya kidijitali ya serikali.

Hatua hizo zinaonyesha dhamira ya eGA ya kuendelea kutumia ubunifu na tafiti za teknolojia za kisasa katika kuboresha huduma za serikali na kuifanya Tanzania kwenda sambamba na maendeleo ya kidijitali duniani.

Mpangilio