e-GA yataja mafanikio ya Ilani ya CCM 2020 – 2025

Taasisi za Umma zaunganishwa katika Mtandao wa Mawasiliano wa Serikali.
Vituo vya kuhifadhia data vya Serikali (Government Data Centers) vyaboreshwa.
Ujenzi wa Mifumo shirikishi na ya Kisekta
Huduma za Serikali zapatikana Kidijitali
Taasisi za Umma zabadilishana taarifa kidijitali
Miaka mitano sasa inatimia tangu Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), ianze rasmi utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020–2025 katika eneo la ujenzi wa Serikali Mtandao .
Katika kipindi hiki, e-GA imekuwa kinara katika kuongoza mageuzi ya utendaji wa Serikali kupitia TEHAMA ili kuboresha utendaji kazi katika taasisi za umma na utoaji wa huduma kwa umma, zikiwa zinapatikana kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu..
Utekelezaji wa Mikakati thabiti ya IIani ya CCM kwa kipindi hiki cha miaka mitano (chini ya Serikali ya Awamu ya Siti inayoongiozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan), kwa kuwekeza kwenye TEHAMA, ndiko kumeiwezesha e-GA kufikia malengo ya utekelezaji wa Ilani hiyo.
Kupitia Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya Mwaka 2019, e-GA imepewa mamlaka ya kusimamia, kuratibu na kukuza jitihada za Serikali Mtandao Pia, e-GA inawajibika kuitekeleza Ilani ya chama kilichopo madarakani katika eneo la Serikali Mtandao.
Ilani ya CCM ya 2020 - 2025, imebainisha maeneo muhimu ya kipaumbele katika ujenzi wa Serikali Mtandao kuwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya TEHAMA, upanuzi wa mtandao wa intaneti serikalini, huduma za serikali kwa njia ya simu (mGov), vituo vya kuhifadhi taarifa (Data Centers), na mifumo ya kidijitali inayowezesha utendaji bora wa serikali.
Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mhandisi Benedict Ndomba amebainisha kuwa, utekelezaji wa Ilani ya CCM tangu mwaka 2020 – 2025 umeleta mageuzi chanya ya matumizi ya TEHAMA Serikalini na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijiti.
Amebainisha kuwa, moja ya kipaumbele cha Ilani hiyo ni kuimarisha Serikali Mtandao kwa kuboresha ujenzi na upanuzi wa miundombinu shirikishi ya TEHAMA, ambapo e-GA imefanikiwa kujenga na kusimamia mtandao wa mawasiliano Serikalini (Government Communication Network - GovNet) na kuunganisha taasisi za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.
“Kwanza tumeweza kujenga na kusimamia miundombinu shiririkishi ambayo hutumiwa na taasisi zote za umma, lakini pia tumekuwa na uhakika wa upatikanaji wa intaneti, na uwezo wa kufatilia na kubaini ikiwa kuna changamoto mahali na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za Serikali wakati wote kwakuwa sisi ndio tunaosimamia miundombinu hii”, amesema Ndomba.
Ameeleza kuwa, mifumo shirikishi ni moja ya kipaumbele kilichowekwa na ilani ya CCM 2020-2025, ambapo e-GA imefanikiwa kujenga mifumo shirikishi inayotumika katika taasisi za umma ikiwemo Mfumo wa baruapepe Serikalini (Government Mailing System), Mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office), Mfumo wa Usimamizi wa Shughuli za Taasisi (Enterprise Resource Management Suite), Mfumo wa kuomba vibali vya kusafiri nje ya nchi kwa watumishi wa Umma wa e-Vibali, na Mfumo wa Huduma za Serikali kwa njia ya simu ya mkononi (M-Gov).
Ndomba ameeleza kuwa, mifumo hii hutumiwa na taasisi mbalimbali za umma na hivyo kurahisisha utendaji kazi na kuziwezesha taasisi kufikia malengo kwa wakati kwa kuondoa urasimu, sambamba na kuboresha utoaji wa huduma bora kwa umma.
Pia, e-GA imeshirikiana na taasisi mbalimbali za umma kujenga mifumo shirikishi ya kisekta, ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya chama tawala. e-GA kwa Kushirikiana na Ushirika imetengeneza Mfumo wa Vyama vya Ushirika (MUVU) unaowezesha wakulima kufahamu mwenendo wa uuzaji wa mazao yao katika vyama vya USHIRIKA na pia imeshirikiana na Wizara ya Maji kutengeneza Mfumo wa ulipaji wa Ankara za Maji (MAJIIS).
Aidha, e-GA imefanikiwa kujenga Mfumo wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini (Government Enterprise Service Bus), na kuziunganisha taasisi 184, mifumo 221 inayowasiliana na kubadilishana taarifa kwa usalama. Hii ni hatua kubwa katika kupunguza urudufu wa mifumo na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa umma.
“Uwepo wa vituo vya Serikali vya kuhifadhi mifumo (Government Data Centres) imewezesha Serikali kudhibiti taarifa zake katika mazingira salama ambayo ni hatua muhimu katika kufikia na serikali mtandao yenye tija, bila kuwa na mahali salama pa kuhifadhi taarifa zetu, hatuwezi kuwa na Serikali Mtandao yenye tija,” amesema Ndomba.
Ameongeza kuwa, eneo jingine la utekelezaji wa ilani ya CCM ni kuimarisha ulinzi wa mifumo na taarifa za serikali dhidi ya matishio ya usalama wa mtandaoni, kwa kuandaa Mkakati wa Usalama wa Mtandao wa Serikali 2022, kutoa mafunzo ya usalama wa TEHAMA kwa taasisi za umma, kufanya tathmini ya mifumo ya TEHAMA katika taasisi hizo pamoja na kufuatilia usalama wa miundombinu muhimu ya TEHAMA kwa saa 24, siku 7 za wiki.
Ukuaji wa matumizi ya teknolojia mpya nacho ni kipaumbele cha ilani ambapo, e-GA kupitia Kituo chake cha Utafiti na Ubunifu cha Serikali Mtandao (eGovernment Research Innovation and Development Centre -eGOVRIDC), hutoa nafasi kwa vijana wa Kitanzania ya kufanya tafiti na bunifu za teknolojia hizo, ili kutengeneza mifumo itakayorahisisha utoaji wa huduma kwa umma.
“Kupitia kituo hiki, mifumo mbalimbali imetengenezwa na baadhi inatumika katika taasisi za umma ikiwemo mfumo wa uendeshaji vikao kidijitali wa e-Mikutano na Mfumo wa mawasiliano kati ya wananchi na Serikali wa e-Mrejesho,” amefafanua Ndomba.
Aidha, e-GA imesaini mikataba ya ushirikiano na vyuo 14 vya Elimu ya Juu kwa ajili ya tafiti na ubunifu wa kidijitali, ili kuendeleza vipaji vya vijana na kuongeza matumizi ya teknolojia mpya.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, e-GA itaendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya chama kitakachokuwa madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kupitia sehemu ya ujenzi wa serikali mtandao, ili kuchangia katika kujenga Tanzania ya kidijitali inayotumia teknolojia kwa maendeleo ya watu wake kijamii, kiuchumi, na kiutawala. Na sasa Serikali Mtandao si ndoto tena, ni uhalisia unaoonekana.