emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

eGA, TCRA Kuendeleza Ushirikiano katika TEHAMA


eGA, TCRA Kuendeleza Ushirikiano katika TEHAMA


Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zimeahidi kuendeleza ushirikiano katika masuala ya utafiti na ubunifu katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa vijana wanaosoma fani hiyo ili kuwa na wataalamu wa ndani waliobobea katika TEHAMA.

Hayo, yamesemwa Agosti 26, 2022 wakati Wajumbe wa Bodi na Menejimenti ya TCRA ilipofanya ziara katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGovRIDC) kilichopo Ndaki ya Sayansi ya Kompyuta, Habari na Mawasiliano - Chuo Kikuu cha Dodoma kuangalia shughuli mbalimbali za utafiti na ubunifu zinazofanyika katika kituo hicho.

Mwenyekiti wa Bodi-TCRA Dkt. Jones Killimbe alisema kuwa, kwa muda mrefu TCRA imekuwa ikishirikiana na eGA katika uendeshaji wa kituo hicho ili kuchochea matumizi ya TEHAMA hapa nchini. Aidha, lengo la TCRA ni kuhakikisha wananchi hasa vijana wanatumia TEHAMA ili kuleta mageuzi ya kimaendeleo katika utoaji wa huduma kwa umma.

“Ninaipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa kuwaweka vijana hawa pamoja na kuwapatia vitendea kazi na zaidi kuwaweka kambini pamoja ili waweze kujikita zaidi katika utafiti na ubinifu wa mifumo ya TEHAMA yenye tija kwa taifa, jambo hili sisi kama bodi ya TCRA tutawaunga mkono zaidi kwa manufaa ya Taifa kwa jumla”. Alisisitiza Dkt. Killimbe.

Alisema kupitia kituo hicho, eGA imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya watu wenye uelewa wa matumizi ya TEHAMA wakatakaosaidia kujenga uchumi wa kidijitali hapa nchini. Hivyo, aliahidi kuwa TCRA ipo tayari kuendeleza ushirikiano huo ili kufanikisha jitihada za Utafiti na Ubunifu.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Eng. Benedict Ndomba ameishukuru TCRA kwa ushirikiano mkubwa inaotoa katika kufanikisha adhma ya Serikali ya kukuza matumizi ya TEHAMA nchini.

Aidha, Eng. Ndomba alisema kuwa, kwa muda mrefu TCRA imekuwa ikisaidia kituo hicho kwa rasilimali fedha zilizowezesha kuweka mazingira mazuri ya kufanya utafiti na ubunifu wa mifumo ya TEHAMA mathalani Mfumo wa e-Mrejesho, Mfumo wa e-Mikutano, Mfumo wa e-Dodoso na Mfumo wa e-Board ambayo ni muhimu sana Serikalini.

Aidha, Eng. Ndomba alifafanua kuwa, kituo hicho kina wanafunzi 73 na Mamlaka imepanga kuongeza uwezo wa kituo ili kiweze kuchukuwa wanafunzi 300 hadi 500 kwa wakati mmoja ili kuchochea Ubunifu na Utafiti katika utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao.

Mamlaka ya Serikali Mtandao ilianzisha Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) mwaka 2019 kwa lengo kuwa nakuwaweka pamoja vijana wanaosoma fani ya TEHAMA ili waweze kufanya utafiti na ubunifu wa mifumo ya TEHAMA yenye uwezo wa kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.