emblem
Mamlaka ya Serikali Mtandao
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015
ega Logo
Habari
ega-svg-tree

Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano Serikalini, wametakiwa kuhuisha taarifa katika tovuti za taasisi kwa wakati, ili kuhakikisha wananchi na wadau mbalimbali wanapata taarifa sahihi za miradi ya maendeleo na huduma zitolewazo na taasisi kupitia tovuti hizo.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za TEHAMA wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bw. Ricco Boma, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya Usimamizi na Uendeshaji wa Tovuti za Serikali, kwa Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano Serikalini wa Wizara, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mhandisi Benedict Ndomba.

Alisema kuwa, kwakuwa tovuti ni nyenzo muhimu ya utoaji wa taarifa rasmi za Serikali, ni muhimu kwa viongozi hao kuzisimamia vema, na kuhakikisha wanahuisha taarifa za tovuti mara kwa mara, ili wananchi waweze kufahamu mambo muhimu yanayojiri katika Wizara ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano mnao wajibu wa kusimamia tovuti za Wizara zenu kwa kuzingatia misingi na kanuni za taaluma ya habari katika utoaji wa taarifa kupitia tovuti, pamoja na kufanya maboresho ya tovuti hizo pale inapohitajika ili kwenda sambamba na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia”, alifafanua Bw. Ricco.

Alisema kuwa, e-GA imepewa jukumu la kusimamia tovuti za Serikali kwa upande wa kiufundi na kuwa ipo tayari kutoa msaada wakati wowote pale inapohitajika, na kuwataka Wakuu wa Idara na Vitengo vya Habari Serikali, kutekeleza jukumu lao la kuhuisha taarifa katika tovuti zao.

Aliongeza kuwa, ili kuwa na utaratibu wa uanzishaji wa tovuti za Serikali, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, iliandaa miongozo mbalimbali ikiwemo Mwongozo wa Matumizi bora, Sahihi na Salama wa Vifaa, Data na Mifumo ya TEHAMA Serikalini wa mwaka 2022, pamoja na Mwongozo wa Kusimamia na Kuendesha Tovuti za Serikali wa mwaka 2014.

Aliongezea kuwa, lengo kuu la kuandaa miongozo hiyo ni kuongeza matumizi ya TEHAMA katika kuimarisha mifumo ya utoaji habari na huduma kwa wananchi na kuwasisitiza viongozi hao kuzingatia miongozo iliyotolewa, kwa maslahi mapana ya Serikali.

Katika mafunzo hayo, mada mbalimbali zikiwemo Sheria ya Serikali Mtandao, Matumizi ya Teknolojia mbalimbali katika kada ya mawasiliano Serikalini pamoja na Usalama wa tovuti pamoja na mitandao ya kijamii inayotumiwa na Serikali zimetolewa, ili kuwawezesha viongozi hao kuweza kukabiliana na changamoto za kimtandao pindi zinapojitokeza.

Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Ofisi Rais- Mipango na Uwekezaji Ndugu, Raymond Mtani, ameishukuru e-GA kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo amesema yatawajengea uwezo na kuwapa misingi bora ya usimamizi na uendeshaji wa tovuti unaofuata viwango na ubora unaohitajika.

Hadi sasa, e-GA kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za umma imefanikiwa kutengeneza takribani tovuti 500, na hivyo kuwezesha wananchi kupata taarifa za miradi ya maendeleo na shughuli mbalimbali inazozifanya kwa wakati.

Mpangilio