emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

MAAFISA TEHAMA SERIKALINI WATAKIWA KUZINGATIA KANUNI,VIWANGO NA MIONGOZO YA SERIKALI MTANDAO


MAAFISA TEHAMA SERIKALINI WATAKIWA KUZINGATIA KANUNI,VIWANGO NA MIONGOZO YA SERIKALI MTANDAO


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt.Francis Michael amewataka maafisa Tehama katika Taasisi za Umma nchini kuzingatia na kufuata kanuni,viwango na miongozo ya Serikali Mtandao katika utendaji kazi wao.

Dkt.Francis ametoa kauli hiyo Novemba 30,2021 jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya wiki moja kwa maafisa TEHAMA wa Taasisi mbalimbali za umma kuhusu usimamizi wa usalama wa mifumo ya TEHAMA Serikalini yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Amesema eneo la usalama wa mifumo ni muhimu sana hivyo maafisa TEHAMA hawana budi kufanya kazi kwa weledi kwani iwapo eneo hilo halitazingatiwa linaweza kuipeleka nchi katika hatari ya mifumo yake kudukuliwa na wadukuzi.

‘’Nyie ni watu muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu na dunia kwa jumla kwa sababu hivi sasa kwenye dunia ya matumizi ya TEHAMA na tutafika huko tu iwapo mtajizatiti na ili kuepuka mifumo yetu kuingiliwa na wadukuzi na kuwa salama hamna budi kufuata sheria,kanuni,viwango na miongozo ya Serikali Mtandao.’’Alisema.

Aidha, pamoja na mafunzo hayo Dkt.Francis ameitaka eGA kuhakikisha kuwa inazifuatilia Taasisi zilizopata mafunzo kujua iwapo zinzayafania kazi na kama yamekuwa msaada wa kutatua changamoto zilizokuwa zikiwakabili.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa eGA ,Mhandisi Benedict Benny Ndomba amesema kwa mwaka huu wa fedha 2021/22 wamepanga kutoa mafunzo ya aina hiyo kwa Taasisi 200 katika sehemu nne na kwa sasa ni sehemu ya pili na ya kwanza ilifanyika mwezi Septemba mwaka huu.

“Nia ni kujenga na kuongeza uwezo wa Taasisi za umma katika kutekeleza jitihada za Serikali Mtandao ili kuimarisha usalama wa mifumo ya Serikali na kuweza kuboresha utoaji huduma kwa wananchi kwa kutumia TEHAMA.”

Vilevile, Mhandisi Ndomba ametaja maeneo makuu manne ya mafunzo hayo kuwa ni viwango na miongozo ya Serikali Mtandao,Usalama wa mifumo,uendeshaji na utekelezaji wa miradi ya TEHAMA,na namna ya kushughulikia majanga mbalimbali pindi yanapotokea

Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya Serikali Mtandao katika kuzijengea uwezo Taasisi mbalimbali za umma ili ziweze kutoa huduma bora Zaidi kwa kutumia TEHAMA na kwa usalama pia ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa usalama wa mtandao wa Serikali.