emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

MFUMO WA e-BOARD WARAHISISHA SHUGHULI ZA UAANDAAJI WA VIKAO.


MFUMO WA e-BOARD WARAHISISHA SHUGHULI ZA UAANDAAJI WA VIKAO.


Mfumo wa e-board umerahisisha na kuwezesha uratibu wa shughuli zote za uandaaji wa vikao mbalimbali vya bodi na menejimenti katika Halmashauri na Taasisi za Umma.

Mfumo huu wa kidigitali unawezesha sekretarieti kuandaa yatokanayo kwenye kikao, wajumbe kupiga kura na kuwawezesha wajumbe wa menejimenti kutengeneza ripoti za utendaji kazi katika vipindi mbalimbali vya mwaka.

Meneja wa Kituo cha Utafiti na Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGovRIDC) Mamlaka ya Serikali Mtandao Dkt.Eng Jaha Mvulla alisema kuwa, mfumo wa e- board umebeba taswira ya shughuli zote zinazofanyika katika utaratibu wa kawaida wa uandaaji vikao kwa lengo la kuboresha uratibuji wa vikao vya bodi, menejimenti na halmashauri.

“Mfumo unalenga kuwasaidia wahusika wa kuandaa vikao yani sekretarieti katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi pamoja na kuwaongozea ufanisi wajumbe katika utekelezaji wa majukumu yao kupitia TEHAMA” Alifafanua.

Jaha alibainisha kuwa, mfumo wa e board umetengenezwa na kusanifiwa na wataalamu wa ndani kutoka e-GA na umekidhi uhitaji wa mchakato mzima wa uaandaji wa vikao kuanzia kwenye utengenezaji wa ajenda, utumaji wa notisi kwa wajumbe, utengenezaji wa makalablasha ya vikao, uchukuaji wa yatokanoyo, hadidu za rejea, upigaji kura pamoja na ripoti mbalimbali za utekelezaji.

Aliongezea kuwa, e-GA iliazimia kutengeneza mfumo wa eBoard ili kusaidia taasisi za umma kuwa na ufanisi kwenye eneo la kuratibu vikao baada ya kuona uhitaji mkubwa wa matumizi ya TEHAMA kwenye eneo hilo.

“Hadi hivi sasa, takribani taasisi 18 zimekwishajiunga na Mfumo wa e-Board na tunandelea kupokea na kuzifanyia kazi barua za maombi ya kuunganishwa kwenye Mfumo huu kutoka Taasisi mbalimbali za Umma lakini pia nitoe wito kwa taasisi nyingine kutumia mfumo huu ili kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa vikao”, alisisitiza Jaha.