emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

MHE. NDEJEMBI AZITAKA TAASISI ZA UMMA KUSHIRIKIANA NA e-GA


MHE. NDEJEMBI AZITAKA TAASISI ZA UMMA KUSHIRIKIANA NA e-GA


Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb) amezitaka Taasisi za Umma kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) katika kutengeneza Mifumo ya TEHAMA itakayorahisisha utoaji wa huduma bora kwa Wananchi.

Ndejembi alisema hayo jana, wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja kukagua utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Mamlaka, katika Ofisi za e-GA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini zilizopo mkoani Iringa.

Aidha, Ndejembi aliipongeza e-GA kutokana na umahiri wake katika utendaji kazi ikiwemo uwezo wa kubuni, kusanifu na kujenga Mifumo mbalimbali ya TEHAMA ambayo imesaidia kuimarisha utendaji kazi wa Taasisi za Umma pamoja na kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

“Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza kujenga taifa la kidijitali kwa kuhakikisha huduma zote za Kiserikali zinatolewa kwa njia ya kidijitali, na kuwafikia wananchi wote kwa urahisi na haraka”, alisema Ndejembi na kuongeza kuwa;

“Hata hivyo kuna baadhi ya taasisi za umma zimekuwa na ugumu wa kubadilika kuendana na kasi ya Rais, zinataka kujifanyia mambo kienyeji, natoa wito kwa taasisi hizo kuitumia e-GA katika kujenga Mifumo itakayosaidia upatikanaji wa huduma kwa wananchi kwa haraka”.

Ndejembi alizitaja baadhi ya kazi zilizofanywa na e-GA kwa kushirikiana na taasisi nyingine za umma ambazo zimeleta matokeo chanya kwa taifa kuwa ni pamoja na utengenezaji wa Mfumo wa Malipo ya Serikali Kieletroniki (GePG) ambao umesaidia Serikali kufahamu mapato yanayoingia kila siku kwakuwa malipo yote kwa sasa hufanyika kupitia Mfumo huo.

“Baadhi ya maeneo jiografia yake ni ngumu kutoka eneo la makazi au Kijiji kimoja hadi zilipo ofisi za Halmashauri, na hivyo kuwa changamoto kwa wakazi wa maeneo hayo kupata huduma za serikali kwa urahisi Zaidi, hivyo ni vizuri e-GA ikajenga mifumo itakayorahisisha wakazi wa maeneo yenye changamoto kama hizi kupata huduma mahali walipo pasi na kufika ofisini” alisema Ndejembi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba, alisema kuwa e-GA ipo tayari kushirikiana na Taasisi zote za umma katika ujenzi na usamimizi wa Mifumo ya TEHAMA ambayo itasaidia kuboresha utendaji kazi katika Taasisi hizo na utoaji wa hudumma kwa wananchi.

“Tutaendelea kushirikiana na Taasisi za Umma ili kuhakikisha huduma kwa wananchi zinatolewa kwa urahisi, haraka na gharama nafuu pamoja na kuboresha ufanisi na utendaji kazi katika Taasisi hizo”, alisema Ndomba.