emblem
Mamlaka ya Serikali Mtandao
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO/IEC 27001:2022 | ISO 9001: 2015
ega Logo
Habari
ega-svg-tree

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb), ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa juhudi zake za kuendelea kujenga Serikali kidijitali kupitia mifumo mbalimbali inayorahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi katika taasisi za umma.

Mhe. Ridhiwani ametoa pongezi hizo alipofungua Mkutano wa Pili wa Jumuiya za Wataalamu wa Utawala na Rasilimaliwatu (AAPAM) Tawi la Tanzania na kutembelea banda la maonesho la e-GA, lililopo jijini Arusha Mei 6, 2026.

“Ninajivunia sana kila ninapotembelea maonesho na kukuta e-GA ikiwa imeleta suluhisho la changamoto mbalimbali kupitia mifumo ya kidijitali inayosaidia kuboresha utendaji wa taasisi za Serikali na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma,” amesema Mhe. Ridhiwani.

Aidha, amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila taasisi ya Serikali kutumia kikamilifu mifumo ya kielektroniki ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati, kwa urahisi na kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake, Afisa TEHAMA kutoka e-GA, Bi. Khadija Mzenzi, akimwelezea Waziri huyo kuhusu mfumo wa e-Barua, amesema mfumo huo umebuniwa na kusanifiwa na e-GA kwa lengo la kutatua changamoto ya watumishi kushindwa kusoma au kushughulikia baruapepe wanapokuwa katika maeneo yasiyo na huduma ya intaneti.

Bi. Mzenzi amesema mfumo huo unamwezesha mtumiaji kufungua na kusoma baruapepe ambazo tayari alishazipokea na kuzifungua awali hata akiwa nje ya mtandao, jambo linalorahisisha ufuatiliaji wa mawasiliano ya kikazi na kupunguza ucheleweshaji wa huduma kwa wananchi.

Ameongeza kuwa mfumo wa e-Barua pia unaruhusu mtumiaji kuandaa na kutuma baruapepe akiwa katika mazingira yasiyo na mtandao. Ujumbe huo huhifadhiwa kwenye kifaa husika na kutumwa moja kwa moja pindi kifaa kinapopata huduma ya intaneti.

Akifafanua zaidi kuhusu usalama wa mfumo huo, Bi. Mzenzi amesema kuwa mtumishi anayetumia e-Barua anatakiwa kuwa na kifaa kinachoruhusu matumizi ya teknolojia za alama za kibayometriki, ikiwemo utambuzi wa alama za vidole na sura, ili kuimarisha ulinzi na usalama wa taarifa za mtumiaji.

Mfumo wa e-Barua ni miongoni mwa ubunifu wa kidijitali unaoendelezwa na e-GA kwa lengo la kuboresha mawasiliano ya Serikali, kuongeza tija kwa watumishi wa umma na kuharakisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Mpangilio