emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

MRADI WA ‘DIGITAL TANZANIA’ KUIMARISHA HUDUMA ZA KIDIJITALI NCHINI


MRADI WA ‘DIGITAL TANZANIA’ KUIMARISHA HUDUMA ZA KIDIJITALI NCHINI


Mradi wa ‘Digital Tanzania’ unatarajiwa kuimarisha utoaji wa huduma kwa njia ya kidijitali kati ya Serikali, Wananchi pamoja na Wafanyabiashara sambamba na kuchochea uwekezaji katika miradi ya kidijitali nchini.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Eng. Benedict Ndomba alipozungumza na mwandishi wetu kuhusu mradi huo ofisini kwake jijini Dodoma.

Alibainisha kuwa, mradi huo una malengo makuu mawili ambayo ni kuongeza upatikanaji wa huduma za mtandao wa intaneti zenye gharama nafuu na ubora wa juu kwa serikali, wafanyabiashara na wananchi sambamba na kuboresha uwezo wa serikali wa kutoa huduma za umma kidijitali.

“Lengo la pili la mradi huo ni kuchangia upatikanaji wa intaneti na upatikanaji wa huduma za umma kidijitali ili kuwezesha sekta binafsi kuwekeza katika miradi ya kidijitali na kuongeza ajira”, alisema Ndomba.

Kupitia mradi huo e-GA inayo majukumu matatu ambayo ni upanuzi wa mtandao wa serikali, uboreshaji wa vituo vya kuhifadhia data pamoja na masafa ya intaneti ‘bandwith’, ambapo kupitia mradi huo jumla ya vituo 660 vinatarajia kunufaika.

Mei 23, mwaka huu Wawakilishi wa Benki ya Dunia wanaosimamia mradi huo pamoja na wajumbe wa kamati hiyo walikutana ofisi za e-GA Mtumba jijini Dodoma na kufanya kikao cha majadiliano juu ya mradi huo ambao utekelezaji wake unaendelea.

Mradi wa ‘Digital Tanzania’ unaofadhiliwa na benki ya Dunia unatekelezwa kwa usimamizi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Pamoja na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali zinazohusika na TEHAMA ikiwemo e-GA.