emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

OFISI YA TAIFA YA MASHITAKA YATAKIWA KUTUMIA MIFUMO YA TEHAMA KUIMARISHA UTOAJI HAKI KWA WANANCHI


OFISI YA TAIFA YA MASHITAKA YATAKIWA KUTUMIA MIFUMO YA TEHAMA KUIMARISHA UTOAJI HAKI KWA WANANCHI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene, amewataka watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS) kutumia Mfumo wa Kielktroni wa Usimamizi na Uendeshaji wa Kesi za Jinai ujulikanao kama ‘Case Management Information System’ (CMIS), ili kuimarisha utendaji kazi na utoaji haki kwa wananchi.

Simbachawene alitoa kauli hiyo jana wakati akikabidhi mfumo wa CMIS na tovuti ya Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, kwa Naibu Waziri Katiba na Sheria Mhe. Pauline Philipo Gekul, kwenye hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika katika ofisi za NPS jijini Dodoma.

Alisema, mfumo wa CMIS unalenga kurahisisha utendaji kazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtakakatika kushughulikia, kusimamia na kuendesha kesi za jinai ili kuweka uwazi na kupunguza malalamiko kwa wananchi, juu ya maamuzi mbalimbali yanayotolewa na Mahakama.

“Mpaka sasa zaidi ya kesi za jinai 17,411 zimeshasajiliwa katika mfumo huu ambapo kati ya kesi hizo, kesi 7,361 zimeshafika mwisho na kutolewa hukumu na kesi 10,050 zipo katika hatua mbalimbali za maamuzi, haya ni mafanikio makubwa katika kuboresha utendaji kazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka”, alisisitiza.

Alibainisha kuwa, Wizara yake kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imeendelea kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha mifumo ya TEHAMA serikalini inawasiliana na kubadilishana taarifa ambapo, mfumo wa CMIS umekwishaunganishwa kwenye mfumo mkuu wa Serikali unaowezesha mifumo ya TEHAMA serikalini kuwasiliana na kubadilishana taarifa (GovESB).

“Mfumo huu wa CMIS umeshaanza kubadilishana taarifa na mifumo ya baadhi ya taasisi za haki jinai amabazo ni Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Mahakama, na hapa tumetekeleza agizo la Mhe. Rais pamoja na mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai ya kutumia mifumo ya TEHAMA katika utoaji haki”, alisema.

Kwa upande wake Naibu Waziri Katiba na Sheria Mhe. Pauline Philipo Gekul alisema, Sekta ya Sheria imejiwekea malengo thabiti katika kuboresha utendaji kazi wake kwa kutumia mifumo ya TEHAMA kupitia program ya e-justice.

“Mfumo wa CMIS utatuwezesha kupata taarifa za kesi mbalimbali zilizoshughulikiwa na hatua zilizofikia na ni kiungo muhimu katika utekelezaji wa majukumu katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na wadau wote waliopo katika mnyororo mzima wa haki jinai na Sekta ya Sheria kwa ujumla”, alisema.

Aliongeza kuwa, Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kupitia e-GA ili kuhakikisha inajenga mifumo madhubuti ya TEHAMA itakayoimarisha utendaji kazi na kuondoa changamoto mbalimbali za utoaji wa haki zilizopo hivi sasa ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati.

Mfumo wa CMIS umetengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS) ikiwa ni miongoni mwa majukumu ya e-GA ya kuimarisha jitihada za Serikali Mtandao kwa kushirikiana na taasisi za umma.