emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

TENGENI MUDA WA MAISHA BINAFSI KUEPUKA UGONJWA WA AFYA YA AKILI: DR. KWEKA


TENGENI MUDA WA MAISHA BINAFSI KUEPUKA UGONJWA WA AFYA YA AKILI: DR. KWEKA


Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA). wametakiwa kutenga muda wa kutosha kwa ajili ya masuala mbalimbali yanayohusu maisha binafsi, ili kujiepusha na msongo wa mawazo unaoweza kusababisha matatizo ya afya ya akili.

Wito huo umetolewa hivi karibuni na Daktari Bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Garvin Kweka, wakati akitoa elimu ya afya ya akili kwa watumishi wa Mamlaka katika kikao cha watumishi kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Dkt. Kweka alisema kuwa, katika tafiti zilizofanywa na wanasayansi wa afya ya akili, zimebaini kuwa, sababu kubwa za watu wanaojitoa uhai zinatokana na mahusiano mabovu au hafifu na jamii zao na hivyo kupelekea kuchukua maamuzi yasiyokuwa sahihi.

“Ni muhimu kutenga muda kwa ajili ya familia na jamii ili kuweza kujiepusha na athari zinazoweza kujitokeza badaye ikiwemo msongo wa mawazo na hatimaye kupelekea kujiua, ni vizuri kuhakikisha kila mmoja wetu hapa anakuwa na mahusiano mazuri na muda wa kutosha na familia pamoja na jamii yake inayomzunguka”, alisema Dkt. Kweka.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa watumishi kuweka uwiano sawa wa maisha binafsi na ya kazini ili kuweza kujiepusha na matatizo ya afya ya akili nayoweza kujitokeza kutokana na kutokuwepo kwa uwiano sawa wa Maisha ya kazini na binafsi.

“Binadamu ukimfungia ndani unambadilisha hali ya afya yake ya akili anapata mihemko isiyokuwa sahihi, hivyo ili kuweza kukabiliana na msongo wa mawazo mahusiano na jamii ni sehemu muhimu ya afya ya akili” Alisisitiza Dkt. Kweka

Naye Mkaguzi wa ndani wa Mamlaka ya Serikali Mtando Bw. Christopher Kambo alisema kuwa, elimu ya afya ya akili iliyotolewa na mtaalamu huyo, imewasaidia kutambua umuhimu wa kuchangamana na jamii ili kuweza kujiepusha na matatizo ya afya ya akili ikiwemo msongo wa mawazo.

Bw. Kambo alisema kuwa, asilimia kubwa ya watumishi katika maeneo mbalimbali wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kutekeleza majukumu ya kikazi na hivyo kusahau kutenga muda wa kutosha kwa ajili ya familia na jamii jambo linaloweza kusababisha msongo wa mawazo.

“Elimu tuliyopewa kuhusu afya ya akili imetusaidia kutambua na kuweka uwiano sawa wa utekelezaji wa majukumu ya Taasisi na maisha binafsi, lakini pia namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku ya kikazi”, alisisitiza Bw. Kambo.

Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imekuwa na utaratibu wa kutoa elimu ya afya ya akili kwa watumishi wake mara kwa mara ili kuhakikisha wanapata elimu sahihi juu ya magonjwa mbalimbali ukiwemo ugonjwa wa afya ya akili ili waweze kuuzuia au kukabiliana nao katika hatua za awali kabla haujaleta madhara.