emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Tumieni Mfumo wa Pamoja Kutoa Ankara za Maji- Mhandisi Fumbe


Tumieni Mfumo wa Pamoja Kutoa Ankara za Maji- Mhandisi Fumbe


Mamlaka za Maji nchini zimetakiwa kutumia mfumo mpya wa pamoja wa utoaji Ankara za Maji (Maji intergrated and unified Billing System) ili kurahisisha uendeshaji, usimamizi na kuongeza mapato ya Mamlaka za Maji.

Hayo, yamesemwa na Mhandisi, Jeremia Fumbe kutoka Wizara ya Maji Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, wakati wa mafunzo ya namna ya kuutumia mfumo huo kwa Maafisa mbalimbali kutoka Mamlaka za maji nchini yanayotolewa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) na kufanyika Mkoani Morogoro kuanzia 10-18 Novemba, 2020.

“Wizara kwa kushirikiana na eGA zinafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha mfumo huu, baada ya kujiridhisha na ufanisi wa mfumo huo, mfumo utaingizwa katika mwongozo wa uendeshaji wa Mamlaka za Maji nchini ili matumizi yake yawe ni sehemu ya matakwa ya kisheria kwa Mamlaka zote za Maji nchini” amesema Mhandisi Fumbe.

Ameongeza kuwa, matumizi ya mfumo huu ni muhimu sana kwa kuwa suala la utoaji huduma na ukusanyaji mapato yatafanyika kwa ufanisi na kuleta tija kwa taifa. Aidha, Mamlaka zote za Maji zinapaswa kutumia mfumo huu na kwa zile zilizokuwa na mifumo mingine hapo awali watatakiwa kuiacha na wale wasiokuwa na mifumo watatakiwa kuanza kutumia mfumo huo.

Mhandisi Fumbe amesema mfumo huo pia una faida nyingi kuanzia kwa mwananchi, Mamlaka hadi Serikali kwa jumla, kwani ni mfumo wa uwazi hivyo unatarajiwa kuongeza ufanisi na kuondoa mianya ya rushwa kwa baadhi ya watendaji wasio waaminifu.

Amebainisha kuwa, katika mfumo kuna sehemu inayomruhusu mwananchi kutuma maombi ya kuunganishwa na huduma ya maji bila hata kufika katika Mamlaka ya maji husika na anaweza kufanya kila kitu akiwa nyumbani tu.

Aidha, Wizara inauwezo wa kuona iwapo mteja amecheleweshewa huduma na hivyo, kuhoji na kutoa maelekezo kwa Mamlaka kutekeleza ombi la mteja haraka. Hii, inaziba kabisa mianya ya rushwa na inaongeza ufanisi wa utendaji.

Naye, Meneja wa TEHAMA kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Mtumwa Simba, amesema mfumo huo una umuhimu mkubwa sana kwao kama wasimamizi na wadhibiti wa huduma hizo za Maji kwani utasaidia kupata taarifa sahihi kutoka kwa Mamlaka hizo sambamba na kufanya ukaguzi kabla kufika katika Mamlaka hizo kwa kutumia mfumo huo.

“Kusakinishwa kwa mfumo huu katika Mamlaka za Maji ambazo zinasimamiwa na EWURA ni hatua muhimu kwa kuwa watalaamu wetu watajifunza kutumia mfumo mmoja tu na kutoa huduma kwa Mamlaka zote. Hii pia itaondoa changamoto ambazo zimekuwa zinajitokeza kwa kuwa na mifumo mingi kiasi kwamba wataalamu wetu wanashindwa kutambua haraka mfumo ulio na tatizo na kulitatua” alisema Simba.

Ameongeza kuwa, mfumo huo utawawezesha wateja kupata huduma za maji kwa kutumia simu zao za mkononi wakiwa mahala popote hivyo kulipa bili za maji mapema na hivyo kuongeza mapato na kupunguza gharama za uendeshaji za mamlaka za maji.

Vilevile, Mratibu wa Mfumo huo kutoka Kitengo cha TEHAMA Wizara ya Maji Mhandisi Masoud Almas amesema mfumo huo utatumiwa na taasisi za maji zote zilizopo chini ya Wizara. Kwa hiyo mafunzo haya ni mahususi kwao kwa kuwa mfumo utasakinishwa katika maeneo yao ya kazi.

“Tunaipongeza Serikali kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kubuni, kusanifu na kutengeneza mfumo ambao utatatua changamoto mbalimbali na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wetu wa kila siku” alisema Almas.

Amebainisha kuwa, mifumo iliyokuwepo hapo awali ilikuwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na mifumo hiyo kutowasiliana hivyo haikuwa rahisi kupata taarifa za pamoja ili uweze kuzifanyia kazi. Pia ilikuwa ikitokea tatizo kupata msaada wa kiufundi ilikuwa ni shida.

Aprili Mosi mwaka 2019 Wizara ya Maji iliingia Mkataba na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kutengeneza mfumo ambapo Aprili hadi Juni 2020 jumla ya Mamlaka tano zilianza kutumia mfumo huo kwa hatua ya Majaribio. Mafanikio yaliyopatikana kumeifanya Wizara kutoa mafunzo kwa taasisi zote za Maji zilizo chini yake ili kuanza kutumia mfumo huo.