emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

USHIRIKISHWAJI WA WATU WENYE ULEMAVU WACHANGIA UBORESHAJI WA HUDUMA JUMUISHI


USHIRIKISHWAJI WA WATU WENYE ULEMAVU WACHANGIA UBORESHAJI WA HUDUMA JUMUISHI


Ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika makongamano na mikutano ya kitaaluma, umetajwa kuwa chachu ya uboreshaji wa huduma jumuishi kwa makundi maalumu.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani Bw. Suleiman Zalala, alipotoa salamu za shukurani wakati wa kilele cha Kikao Kazi cha Nne cha Serikali Mtandao kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) uliopo jijini Arusha Februari 8 mwaka huu.

“Huu ni mwaka ya pili tunashiriki katika kikao cha aina hii, e-GA imetuthamini kwakuona umuhimu na mchango wa kundi hili maalumu kushiriki katika kikao kazi cha Nne cha Serikali Mtandao, ili kupata nafasi ya kukutana na wadau mbalimbali wa TEHAMA sambamba na kuwasilisha changamoto tulizonazo na mahitaji yetu ili kuboresha huduma jumuishi za Serikali Mtandao kwa watu wenye ulemavu”, alisema Zalala.

Aliongeza kuwa, ni wakati sahihi kwa Taasisi nyingine za Umma na binafsi kutowaacha nyuma watu wenye ulemavu kwa kuiga mfano mzuri wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), wa kuhusisha makundi maalumu kwenye makongamano pamoja na mafunzo mbalimbali wanayoyaandaa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Eng. Benedict Ndomba, aliahidi kuendeleza ushirikiano na makundi maalumu ikiwemo CHAVITA, ili kuhakikisha utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao unachagiza maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa makundi yote muhimu ya kijamii.

Alibainisha kuwa, e-GA itaendelea kushirikiana na makundi maalum sambamba na kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao ili kuhakikisha Serikali Mtandao inaleta manufaa kwa watu wote wenye ulemavu na wasiokuwa na ulemavu.

“Serikali Mtandao inalenga kurahisisha utoaji na upatikanaji wa huduma za Serikali kwa wananchi mahali walipo na kwa gharama nafuu sisi e-GA tunadhamiria kuhakikisha makundi yote ya kijamii wakiwemo walemavu wananufaika na Serikali Mtandao”, alisema Ndomba.

Kikao Kazi cha Nne cha Serikali Mtandao kiliongozwa na kaulimbiu isemayo uzingatiwaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa Ubadilishanaji Salama wa Taarifa na kuwakutanisha takribani Zaidi ya wadau 1000 kutoka katika Taasisi, na Mashirika ya Umma.