Wadau wa Serikali Mtandao Kukutana Arusha Februari 2026

Wadau wa Serikali Mtandao kutoka katika sekta mbalimbali ndani na nje ya nchi, wanatarajia kukutana jijini Arusha mapema mwezi Februari mwaka 2026 katika mkutano wa sita (6) wa Serikali Mtandao.
Takribani wadau zaidi ya 1000 kutoka katika taasisi na mashirika mbalimbali ya umma nchini, pamoja na wageni kutoka nje ya Tanzania, wanatarajiwa kukutana katika mkutano huo utakaofanyika tarehe 10 hadi12 Februari, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), jijini Arusha,.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba amesema, mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka katika kuratibu, kusimamia, kuendeleza na kukuza jitihada za Serikali Mtandao nchini, sambamba na kuimarisha ushirikiano baina ya e-GA na wadau wake.

“Hili ni jukwaa muhimu linalowakutanisha wataalamu, viongozi na watumiaji wakuu wa mifumo ya Serikali Mtandao ili kujadili mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizopo, na namna bora ya kuimarisha zaidi utoaji wa huduma za umma kwa njia ya TEHAMA,” amesema Ndomba.
Ndomba amebainisha kuwa, Mgeni rasmi wa mkutano huo anatarajiwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi Ndg. Balozi Moses Kusiluka. Aidha, mkutano utaongozwa na kaulimbiu isemayo:“Kuboresha Utendaji wa Serikali kwa Kuimarisha Utoaji wa Huduma za Umma Kupitia Mifumo Salama na Jumuishi ya Serikali Mtandao.”
Kaulimbiu hiyo inasadifu uelekeo wa Serikali katika kuhakikisha kuwa mifumo ya TEHAMA inayojengwa serikalini, inakuwa Madhubuti na salama ii iweze kutumika kwa usahihi na kuleta tija kwa wananchi, kuongeza uwajibikaji, usalama wa taarifa, na kurahisisha utoaji wa huduma mbalimbali za umma.
Mhandisi Ndomba amewataka wadau wote wa serikali mtandao wakiwemo Maafisa Masuuli, Wakurugenzi, Wakuu wa TEHAMA, Maafisa Mawasiliano, Mipango, Fedha, Rasilimali Watu, Manunuzi, Watunza Kumbukumbu, pamoja na Watumiaji wote wa mifumo ya TEHAMA serikaini, kushiriki kikamilifu katika mkutano huo.
“Uwepo wa makundi haya ni chachu katika kukuza jitihada za Serikali Mtandao, kwa sababu wao ndio watumiaji wakuu wa mifumo, hivyo majadiliano yatakayofanyika katika mkutano huo yatasaidia kuongeza uelewa wa pamoja na kuimarisha utendaji katika taasisi zao.” amefafanua Mhandisi Ndomba.
Kwa upande wake Meneja wa Mawasiliano wa e-GA, Bi. Subira Kaswaga, ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya mkutano huo, amethibitisha kuwa, taratibu zote muhimu zinaendelea vizuri, ikiwa ni pamoja na maandalizi ya ukumbi, ratiba pamoja na Mfumo wa usajili wa washiriki wa TSMS.



