emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

WANAFUNZI KUTOKA KITUO CHA UTAFITI NA UBUNIFU WATEMBELEA MAKAO MAKUU YA e-GA


WANAFUNZI KUTOKA KITUO CHA UTAFITI NA UBUNIFU WATEMBELEA MAKAO MAKUU YA e-GA


Wanafunzi 55 kutoka Vyuo Vikuu 11 nchini waliopo katika programu maalumu ya mafunzo kwa vitendo inayoendeshwa na Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) wametembelea Makao Makuu ya e-GA yaliyopo Mtumba jijini Dodoma Septemba 08, 2023.

Akipokea ugeni huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Mkurugenzi wa Huduma na Uwezeshaji wa e-GA Bw.Salum Mussa amewataka vijana hao kutumia uzoefu walioupata katika kituo hicho kubuni mifumo na aplikesheni zitakazoweza kutatua changamoto zilizopo katika jamii.

“Tunaandaa mazingira ya kuja kuwatembelea tukiwa na viongozi wengine, tunatarajia tukija huko kituoni mtuoneshe kwa vitendo kile mlichokipata kutokana na program hii.” Amesema Bw. Salum.

Kwa mujibu wa Meneja wa e-GovRIDC Dkt. Jaha Mvula amesema kuwa program hiyo ya wiki 10 ilianza tarehe 22 Julai,2023 na inatarajia kukamilika mwanzoni mwa mwezi Oktoba.

“Lengo kubwa ni kuwapa fursa wanafunzi wa kada ya TEHAMA kupata picha halisi ya masomo wanayoyasoma pamoja na hali halisi ya sekta husika ilivyo. Hivyo, program hii inawajengea uwezo wanafunzi hawa na kuchochea ubunifu na vipaji vyao.” Amefafanua.

Dkt. Mvula ameongeza kuwa katika muda ambao wanafunzi hao walikuwa katika kituo hicho wamejikita zaidi katika kutengeneza mifumo ya kompyuta na applikesheni mbalimbali, uendelezaji wa akili bandia (Artificial intelligence) na mifumo ya fedha za mtandao (Blockchain) na usalama mtandaoni (Cybersecurity).