emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

WANAFUNZI WATAKIWA KUTUMIA TEKNOLOJIA MPYA KULETA MAGEUZI YA KIDIJITALI SERIKALINI


WANAFUNZI WATAKIWA KUTUMIA TEKNOLOJIA MPYA KULETA MAGEUZI YA KIDIJITALI SERIKALINI


Wanafunzi wanaofanya mafunzo kwa vitendo katika tasnia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), wametakiwa kuwa wabunifu katika kutumia teknolojia mpya zilizoibuka duniani ili kuongeza ufanisi na kuleta tija katika utendaji wa shughuli mbalimbali za Serikali.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mha. Benedict Ndomba, wakati akifungua mafunzo ya awamu ya tano katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGovRIDC) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao.

Alisema kuwa, teknolojia mpya zimeibuka duniani kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, zikiwemo Akili Bandia (Artificial Intelligence), Sarafu ya Kidijitali (Digital Currency), Block Chain, Usalama wa Mtandao (Cyber Security) na Internet of Things (IOT), hivyo ujuzi mkubwa unahitajika katika kuzielewa teknolojia hizo na kuzitumia ili kuleta mageuzi makubwa ya Serikali Mtandao.

“Kutokana na teknolojia mpya Serikali haina budi kwenda sambamba na uelekeo wa dunia kwa kuangalia matumizi sahihi ya teknolojia hizo, katika utendaji wa shughuli za Serikali lakini pia katika utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi”, alisema Ndomba.

Mamlaka ya Serikali Mtandao, inatarajia kuwa mafunzo kwa vitendo yanayotolewa katika kituo hicho, yatawasaidia wanafunzi kuongeza ujuzi na uzoefu katika kuzielewa teknolojia mpya ili kuchochea maendeleo na mageuzi makubwa ya Serikali ya kidigitali, alisisitiza Ndomba.

Aidha, Ndomba aliwataka wanafunzi hao kuwa mabalozi wazuri na kuzingatia mafunzo yanayotolewa kwa kutumia vizuri nafasi walizopata kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Aliongezea kuwa, Mamlaka imejiandaa na kuweka mazingira mazuri ya mafunzo kwa lengo la kuhakikisha uwepo wa mazingira rafiki na salama ili kuepusha usumbufu wa aina yeyote katika kipindi chote cha mafunzo hayo.

Naye Meneja wa Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGovRIDC) Dkt. Jaha Mvulla, alisema e-GA imejipanga kushirikiana na wataalamu kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na sekta binafsi zikiwemo Vodacom, NMB na Citi Benki, katika kutoa mafunzo hayo ili kuhakikisha vijana wanapata uzoefu wa kutosha pamoja na kufahamu mambo muhimu yanayohitajika katika sekta ya TEHAMA.

Wanafunzi wanaopata mafunzo hayo wameipongeza na kuishukuru e-GA kwa kupata fursa ya kuchaguliwa kushiriki katika mafunzo hayo ambayo yatawasaidia kuongeza ujuzi na uzoefu katika matumizi ya teknolojia mpya zilizopo duniani.

Bw. Khamis Khemed mwanafunzi wa mwaka wa kwanza (1) katika Chuo cha Taifa Zanzibar, alisema kuchaguliwa kwake kushiriki katika mafunzo hayo kunatokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania Bara na Visiwani katika kuchochea na kukuza Jitihada za Serikali Mtandao baina ya pande zote mbili.

“Mafunzo haya ni muhimu kwani nitaweza kujifunza mifumo mbalimbali na teknolojia mpya zilizoibuka na namna ya kutumia teknolojia hizo ili kuleta tija kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, lakini pia uwepo wangu hapa unadhihirisha ushirikiano imara uliopo bara na visiwani katika kuimarisha Serikali Mtandao” Alisema Bw. Khemed

Bw. Khemed ameiomba Serikali kuendelea kuisadia e-GA katika shughuli mbalimbali za utafiti na ubunifu ili kuchochea mageuzi ya Serikali kidijitali na hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji kazi katika taasisi za umma.

Naye Bi. Maseil Mussa, mwanafunzi wa mwaka wa tatu (3) Chuo Kikuu Cha Dodoma alisema, mafunzo hayo yatawasaidia kuweza kuzielewa teknolojia mpya na kutumia teknolojia hizo katika uvumbuzi wa mifumo mbalimbali itakayosaidia Serikali katika utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Wanafunzi mbalimbali wa fani ya TEHAMA kutoka vyuo vikuu kumi na moja (11) vya Tanzania bara na Visiwani wanashiriki mafunzo hayo kwa muda wa wiki kumi (10), ambapo wanafunzi hao walichaguliwa kushiriki mafunzo hayo baada ya kutuma maombi kupitia mfumo wa Ubunifu Portal.