emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

WAZIRI AWATAKA WANAFUNZI WANAOFANYA MAFUNZO KWA VITENDO KUWA WABUNIFU, WAADILIFU NA WAZALENDO


WAZIRI AWATAKA WANAFUNZI WANAOFANYA MAFUNZO KWA VITENDO KUWA WABUNIFU, WAADILIFU NA WAZALENDO


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama amewataka wanafunzi wanaofanya mafunzo kwa vitendo kutumia fursa waliyoipata vizuri kwa kuwa wabunifu, waadilifu na wazalendo kwa kubuni mifumo ya kimkakati itakayosaidia Serikali kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.

Mhe. Waziri amesema hayo tarehe Agosti 10, 2022 wakati alipotembelea Ofisi za Mamlaka ya Serikali Mtandao katika kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGovRIDC) kilichopo Ndaki ya Sayansi ya Kompyuta, Habari na Mawasiliano - Chuo Kikuu cha Dodoma.

Mhe. Waziri Mhagama ameongeza kuwa ujenzi wa kituo cha utafiti utachochea ari ya vijana kujifunza kwa vitendo na kuchangia katika ustawi wa taifa kupitia tafiti mbalimbali zinazofanywa hasa katika utatuzi wa changamoto mbalimbali katika jamii na kuibua vipaji ambavyo vitasaidia kuleta maendeleo na kuimarisha mahusiano mazuri ndani na nje ya nchi.

“Ninaitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao kutafuta rasilimali fedha na kuweka mpango wa kimkakati wa namna ya kuongeza idadi ya vijana wanaokuja kufanya mafunzo kwa vitendo katika masuala ya TEHAMA ili kuchochea utafiti na ubunifu” amesema Mhe. Mhagama.

Ameongeza kuwa endapo utafiti na ubunifu utaimarika, Serikali itakuwa na mifumo ya kimkakati na kutakuwa na suala la ukusanyaji wa mapato litakuwa rahisi, mazingira ya uwekezaji na biashara yataimarika, usimamizi wa fedha za umma na utakuwa umeboreshwa na kutakuwa na upatikanaji wa huduma bora kwa umma kwa wakati na kwa gharama nafuu.

Mhe. Mhagama amesema utekelezaji wa mifumo hii uende sambamba nausimamizi wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo iliyowekwa ili kuhakikisha Jitihada za utekelezaji wa Serikali Mtandao zinaonekana na kufikia lengo la kuwa na uchumi wa kidijitali.

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa Juhudi kubwa wanazofanya katika utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao nchini,

Amesema Mamlaka kupitia wanafunzi hao imefanya kazi kubwa ya utafiti na ubunifu wa mifumo inayowezesha Serikali kutatua changamoto mbalimbali za kisekta na kukuza matumizi ya TEHAMA nchini.

“Nawapongeza Mamlaka, kama Serikali tunatambua mnachokifanya na tunawatia moyo kama nchi tumesogea mbele na tunahitaji kusonga mbele zaidi katika masuala ya TEHAMA”

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Eng. Benedict Ndomba amesema suala la Utafiti na Ubunifu ni la msingi na linasaidia kwa kiasi kikubwa kuendeleza jitihada za Serikali Mtandao katika maeneo mbalimbali kama vile ujenzi, usimamizi na uendeshaji wa mifumo na miundombinu ya serikali mtandao.

Eng. Ndomba amesema Mamlaka imefanikiwa kuongeza idadi ya wanafunzi wa mazoezi waliopita katika Kituo hicho kutoka idadi ya wanafunzi 33 katika awamu ya kwanza hadi kufika wanafunzi 72 katika awamu ya pili.

Kwa sasa, Eng. Ndomba amesema Mamlaka imepanga kuongeza uwezo wa Kituo ili kiweze kuchukuwa wanafunzi 300 hadi 500 kwa wakati mmoja ili kuchochea Ubunifu na Utafiti katika utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao.

Mamlaka ya Serikali Mtandao ilianzisha Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) mwaka 2019 kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa umma kupitia utafiti na kufanya ubunifu katika maeneo mbalimbali