emblem
Mamlaka ya Serikali Mtandao
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO/IEC 27001:2022 | ISO 9001: 2015
ega Logo
Habari
ega-svg-tree

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imeendelea kupiga hatua kubwa katika kuimarisha usalama wa mifumo ya TEHAMA, kuongeza ufanisi wa huduma za kidijitali na kuunganisha taasisi za umma katika mfumo mmoja jumuishi ili kuchochea na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Hayo yameelezwa Aprili 17, 2026 Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani J. Kikwete, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Waziri Kikwete alibainisha kuwa,katika kuhakikisha mifumo ya Serikali inakuwa salama wakati wote wa matumizi,e-GA imebuni na kuwezesha mfumo wa usalama wa kitaifa wa ulinzi wa mifumo ya Serikali ujulikano kwa jina la  NGAO.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfumo wa Ngao  umeanza kutumika kwa mafanikio, ambapo taasisi na vituo vya huduma 723 tayari vimejiunga. Serikali inalenga kuhakikisha taasisi zote 780 zinazotumia mfumo wa baruapepe Serikalini (Goverment Mailing System- GMS) zinaunganishwa kwenye mfumo wa Ngao ili kuongeza usalama wa taarifa za Serikali.” Waziri Kikwete aliliambia Bunge.

Sanjari na hilo,Waziri Kikwete ameliambia Bunge kwamba katika kipindi hicho tajwa, tathmini ya usalama imefanyika kwa mifumo 355 inayopatikana mtandaoni kati ya mifumo 450 iliyopangwa kufanyiwa tathmini.

Aidha, tathmini ya uzingatiaji wa viwango na miongozo ya usalama wa Serikali Mtandao imefanyika katika taasisi 91 kati ya taasisi 150 zilizopangwa kufanyiwa tathmini kwa lengo la kuhakikisha kuwa mifumo na miundombinu ya TEHAMA Serikalini inafanya kazi kwa ufanisi, na kutoa huduma bora, salama, na endelevu kwa wananchi.

Waziri Kikwete aliliambia Bunge kwamba Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuongeza na kuboresha ufanisi kwenye miundombinu  ya TEHAMA nchini ikiwemo ununuzi na uboreshaji wa seva za kuhifadhi data, kuimarisha mifumo ya umeme wa dharura, pamoja na kuboresha vituo vya kuhifadhi taarifa.

Pia Serikali kupitia e-GA ilifanya uhuishaji wa miundombinu ya vituo vya kuhifadhi data na taarifa kwa kununua vifaa vya TEHAMA, kuboresha mfumo wa umeme wa dharura (power backup), kununua vifaa vya miundombinu ya kangavuke (generator) kwa ajili ya kuwezesha mifumo ya kiotomatiki kufanya kazi .

Kadhalika Waziri Kikwete alisema kuwa, Serikali kupitia e-GA imeendelea kupanua huduma za Serikali Mtandao kwa kuunganisha mifumo mbalimbali kupitia Mfumo wa Pamoja wa Ubadilishanaji wa Taarifa Serikalini (GovESB), ambapo hadi kufikia Machi 2026 jumla ya mifumo 252 kutoka taasisi 200 imeunganishwa.

Mifumo hiyo inahusisha sekta muhimu ikiwemo Mahakama, Polisi, TAKUKURU na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambazo zimewezeshwa na mfumo kuwasiliana na kubadilishana taarifa ili kurahisisha utendaji kazi wa kila siku.

“ Mheshimiwa Mwenyekiti,kwa upande mwingine, juhudi zimefanyika katika kuunganisha taasisi 660 kwenye mtandao wa mawasiliano wa Serikali (Government Network), pamoja na kuanzisha na kuboresha mifumo mbalimbali ikiwemo e-Office, e-Mrejesho, e-Ukaguzi na e-Mikutano ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma kwa wananchi." Alisema Waziri Kikwete.

Pamoja na hayo,Waziri Kikwete pia aliliambia Bunge kuhusu mafanikio mbalimbali ambayo Serikali imeyapata ndani na nje ya nchi katika utekelezaji wa afua za Serikali Mtandao.

Kikwete, alibainisha kuwa Tanzania imepata kutambuliwa kimataifa kufuatia ubunifu na matumizi madhubuti ya mifumo ya Serikali Mtandao.

 Alieleza kuwa mfumo wa e-Mrejesho toleo la pili (e-Mrejesho v2) umeiwezesha nchi kushinda tuzo ya World Summit on the Information Society 2025 (WSIS Grand Champion), tuzo inayotolewa kwa miradi bunifu ya TEHAMA duniani.

Mbali na mafanikio hayo, Waziri Kikwete alibainisha kuwa Tanzania imeorodheshwa katika Kundi A la nchi zenye ukomavu wa juu wa matumizi ya teknolojia serikalini (Extensive GovTech Maturity), kwa mujibu wa tathmini ya Benki ya Dunia.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio haya yanaonesha juhudi za Serikali katika kuimarisha huduma za kidijitali na ushirikishwaji wa wananchi.Kwa ujumla, mafanikio haya yanaonesha dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kujenga mfumo imara wa Serikali Mtandao unaolenga kutoa huduma bora, salama na za haraka kwa wananchi.” Alifafanua Waziri Kikwete.

Mpangilio