emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

WAZIRI MHE. JENISTA MHAGAMA AZINDUA BODI YA WAKURUGENZI e-GA


WAZIRI  MHE. JENISTA MHAGAMA AZINDUA BODI YA WAKURUGENZI e-GA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora Mhe.Jenista Mhagama (Mb), ameitaka Bodi ya Wakurungezi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, sambamba na kuwajengea uelewa wadau mbalimbali kuhusu dhana na umuhimu wa Serikali Mtandao kwa ustawi wa Taifa.

Waziri Mhagama ameyasema hayo Novemba 25 mwaka huu wakati akizindiua Bodi hiyo katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi za e-GA Kanda ya Dar es Salaam, na kuwataka wajumbe wa bodi kuzingatia uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja na kushirikiana na Menejimenti ya e-GA katika kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza.

“Katika kutekeleza majukumu yenu mtakutana na changamoto mbalimbali ambazo e-GA imekuwa ikikabiliana nazo ikiwemo kuwepo kwa Mifumo ambayo haijumuishi taratibu za utendaji kazi (business processes) kuanzia mwanzo hadi mwisho (end-to-end) katika baadhi ya Taasisi za Umma jambo linalopelekea taratibu nyingine kufanyika nje ya Mfumo au kwa kutumia Mifumo mingine isiyowasiliana” alisema Waziri Mhagama.

Aidha, Waziri Mhagama alizitaja changamoto nyingine zinazoikabili e-GA kuwa ni upungufu wa wataalamu waliobobea katika usanifu, ujenzi na uendeshaji wa Mifumo na miundombinu pamoja na usalama wa TEHAMA katika Taasisi za Umma, kuongezeka kwa matishio ya usalama wa Mtandao pamoja na mabadiliko ya haraka ya Teknolojia.

Vilevile, Waziri Mhagama alisema kuwa, Bodi hiyo inaanza kazi katika kipindi ambacho mahitaji ya Serikali Mtandao ni makubwa hivyo, anatarajia kuwa Bodi itashiriki kikamilifu katika kutoa ushauri na kutekeleza majukumu yake vema ili kujenga Serikali ya kidigitali.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Xavier Daudi alisema kuwa, Wizara inahakikisha utekelezaji wa Serikali Mtandao unafanyika kwa usahihi, usalama na kwa kuzingatia miongozo ya Kisera.

Katika kufanikisha hayo, Wizara imeandaa Mkakati wa Serikali Mtandao (e-Government Strategy 2022) na Mkakati wa Serikali wa Kuzuia/Kukabiliana na Uhalifu wa Kimtandao (Government Cyber Security Strategy 2022) ili kuweka dira mahususi katika kutekeleza jitihada za Serikali Mtandao, alisema Naibu Waziri na kusisitiza kuwa,

“Ninaielekeza Bodi hii kuhakikisha nyaraka hizi zinazingatiwa ipasavyo ili tuweze kufikia malengo tarajiwa ya kuwa na matumizi sahihi ya Serikali Mtandao, na hatimaye kuboresha utendaji kazi Serikalini na utoaji wa huduma kwa umma”.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya e-GA Dkt.Mussa Kissaka amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua yeye pamoja na Waziri Mhagama kuwateua wajumbe wa Bodi na kuahidi kutoa ushirikiano kwa Wizara pamoja na Menejimenti ya e-GA ili kuhakikisha Mamlaka inafikia malengo kusudiwa.

“Nimepokea maelekezo ya Waziri na changamoto zote alizozianisha hapa kwa niaba ya wajumbe wa Bodi naahidi kuwa tutazifanyia kazi changamoto na maelekezo hayo ili kuhakikisha utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao unafanikiwa kwa kuzingatia Sera, Sheria na Kanuni zilizopo”, alisema Dkt. Kisaka.

Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao inaundwa kwa Mujibu wa Sheria ya Serikali Mtandao Sura Na. 273, Kifungu namba 7 na kuipa majukumu kupitia Kifungu namba 8.