Waziri Mkuu azindua mfumo wa GoVESB

• Azitaka Taasisi zote za Umma kuijunga na Mfumo huo ifikapo Julai 30
• Asisitiza Taasisi za Umma kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais
• Afurahishwa na faida za Mfumo huo kwa Serikali
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa (Mb), ameziagiza taasisi za umma ambazo bado hazijajiunga na Mfumo wa Kuwasiliana na Kubadilishana Taarifa Serikalini (Government Enterprise Service Bus - GovESB), kujiunga na mfumo huo ifikapo Julai 30 mwaka huu.
Majaliwa ametoa maagizo hayo Juni 23 mwaka huu, alipotoa hotuba kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali park jijini Dodoma.
Alisema kuwa, ni lazima taasisi zote za umma zinazotakiwa kujiunga katika mfumo wa GoVESB kufanya hivyo kabla ya tarehe 30 Julai,ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika kurahisisha upatikanaji wa huduma za Serikali kwa wananchi kidijitali.
“Ni muhimu kujiunga na mfumo wa GovESB, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia alisisitiza kuwa, pindi Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) itakapokamilisha ujenzi wa mfumo huu kila taasisi ipeleke mfumo wake, idadi ya taasisi zilizounganishwa ni chache ukilinganisha na taasisi za Serikali tulizonazo”, alifafanua Mhe.Majaliwa
Aliongeza kuwa, taasisi zote za umma zinapaswa kujiunga na mfumo huo kwani, licha ya kuwa na faida nyingi zinazochagiza kuongezeka kwa ufanisi ndani ya Serikali na kuwezesha utoaji wa huduma bora za Serikali kwa wananchi kwa wakatilakini pia hauna gharama.
“Hakuna sababu ya taasisi yeyote kutoingia katika mfumo huu, na muda ukifika naomba taarifa ya ambao hawajaingia kwenye mfumo huu, ambao watakuwa hawajajiunga na mfumo huu itakuwa ndiyo wala rushwa”, alisema Mhe.Majaliwa.
Aidha, Majaliwa alifurahishwa na jitihada zinazofanywa na e-GA za kutumia wataalamu wazawa katika ujenzi wa mifumo mbalimbali ya TEHAMA Serikalini, jambo ambalo linachangia kukuza vipaji vya wazawa na kuongeza usalama wa mifumo na taarifa za Serikali.
Alisema kuwa, ni muhimu kuwapongeza vijana wote wa kitanzania wanaoshiriki katika ujenzi wa mifumo mbalimbali ya TEHAMA ndani ya Serikali ili kuwapa moyo wa kuendelea kufanya kazi kwa bidii zaidi.
Mhe. Majaliwa alitoa tuzo kwa Maafisa TEHAMA 15 wa e-GA walioshiriki kutengeneza mfumo wa GoVESB na kuwasihi kuendelea kufanya vizuri zaidi katika ujenzi wa mifumo ya TEHAMA katika taasisi za umma.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene (Mb) alisema, matumizi ya mfumo wa GovESB yamepunguza urasimu na msongamano katika ofisi za umma ambazo hubadilishana taarifa kupitia mfumo huo.
“Ubadilishanaji wa taarifa kupitia mfumo huu unaharakisha sana utoaji wa huduma kwa sababu watoaji huduma wote wanasomana hivyo inapunguza adha kwa mwananchi ya kutembea kutoka ofisi moja hadi nyingine ili kupata huduma”, alifafanua Simbachawene.
Tangu kuanza kutumia kwa mfumo wa GoVESB, taasisi za umma zaidi ya 180 zimeunganishwa na mifumo zaidi ya 200 inawasiliana na kubadilishana taarifa. Aidha, e-GA inaendelea na Jitihada za kuhamasisha taasisi za umma kujiunga na mfumo huo.