Afya Bora Huongeza Ufanisi Kazini: Dkt. Hafidh

Na. Catherine Peter
Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), wametakiwa kulinda afya zao ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao kazini.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Dkt. Hafidh Ameir, Afisa anayeratibu Afua za VVU mahali pa kazi ngazi ya taifa, katika Sekta ya Umma kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), wakati wa kikao cha mwaka cha watumishi wa e-GA kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Maji jijini Dodoma.
Dkt. Ameir alisema, afya bora ya mwili na akili huchangia utendaji kazi ulio bora na makini ikiwemo kusimamia na kuendeleza mifumo ya TEHAMA Serikalini, ambalo ni miongoni mwa jukumu kubwa la e-GA, na kuwataka watumishi kuona umuhimu wa kuwekeza katika afya zao.
Alisema watumishi wengi wa Serikali wako katika hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo shinikizo la damu na kisukari, hali inayochangiwa na ulaji wa vyakula visivyozingatia lishe bora.
Sambamba na hilo, ameshauri watumishi kujenga mazoea na utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara ili kujikinga dhidi ya magonjwa nyemelezi na kuishi katika mtindo bora wa maisha
“Watumishi wanapaswa kujenga mazoea ya kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara hata kama hawana dalili zozote za ugonjwa na kuzingatia mlo kamili ikiwemo kujiepusha na vyakula vya viwandani (junk food), ambavyo huchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la magonjwa sugu yasiyoambukiza,” alisisitiza Dkt. Ameir.Top of FormBottom of Form
Alisema watumishi wakiimarisha afya wataweza kuongeza ubunifu, kupunguza utoro unaotokana na maradhi, na kuboresha utoaji wa huduma bora za Serikali kwa wananchi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mhandisi. Benedict Ndomba alimshukuru Dkt. Ameir kwa wasilisho hilo na kuwataka watumishi kuendeleza utamaduni wa kufanya mazoezi ya mara kwa mara na kuzingatia kanuni bora za afya.
“Ni muhimu kila mmoja wetu akachukua hatua za makusudi kulinda afya yake. Mazoezi ya mara kwa mara na mtindo bora wa maisha utatuwezesha kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi zaidi na kuendelea kutoa huduma bora za kidijitali kwa wananchi,” alisema Mhandisi. Ndomba.
Kikao cha Watumishi wa e-GA kilifanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 26 hadi 27 Februari, 2026 na kuhitimishwa na bonanza la michezo Februari 28 katika viwanja vya Kilimani jijini Dodoma. Sambamba na mada ya Afya, pia watumishi walipata elimu kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo taratibu na maadili ya utumishi wa umma, uwekezaji, Usalama mahali pa kazi, mapambano dhidi ya Rushwa na umuhimu wa kuzingatia usalama na usiri wa taarifa za Serikali.



