emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

BADILISHENI MTINDO WA MAISHA KULINDA AFYA ZENU


BADILISHENI MTINDO WA MAISHA KULINDA AFYA ZENU


Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) wametakiwa kubadili mtindo wa maisha ili kuwa na afya bora.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Rasilimali Watu na Utawala Bw. Eric Kalembo katika zoezi la upimaji afya za watumishi lililofanyika katika Ofisi za Mamlaka ya Serikali Mtandao, jijini Dar Es Salaam.

Bw. Kalembo amesema kuwa Idadi kubwa ya watumishi wa Mamlaka ni vijana ambao ni chachu ya maendeleo ya Taifa hivyo wanapaswa kuwa na afya bora.

Bw. Kalembo amesema Mamlaka ya Serikali Mtandao imewekeza katika afya bora za watumishi kwa kuweka utaratibu wa kuhakikisha wanapima afya zao mara kwa mara na kupatiwa matibabu sahihi pindi inapohitajika.

“Zoezi hili la upimaji wa afya ni mojawapo ya maazimio ya Kamati ya VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukiza ya Mamlaka inayowataka watumishi wote kupimwa afya zao na kupatiwa matibabu kwa wakati ili waweze kutekeleza majukumu yao vyema” amesema Kalembo.

Meneja ametoa rai kwa Watumishi wote wa Umma kuhakikisha kuwa wanapima afya zao na kupatiwa ushauri nasaha kwani magonjwa yasiyoambukiza ni tishio kubwa duniani.

Naye Dkt. Richard Vyagasa mtaalamu wa Afya kutoka Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) amesema kuwa OSHA inasimamia na kuhakikisha kuwa watumishi wanafanya kazi katika mazingira salama na huduma mbalimbali za kuboresha afya za Watumishi sehemu ya kazi zinazingatiwa.

“OSHA inafanya ukaguzi wa vitendea kazi vya watumishi, kuhakikisha mwanga wa taa ni sahihi katika maeneo ya kazi, muundo wa ofisi pamoja na afya bora kwa ujumla kwa watumishi hivyo zoezi hili litakapokamilika taarifa itaandaliwa na kuwasilishwa kwa uongozi wa e-GA pamoja na mapendekezo ya kuboresha afya za watumishi” Alisema Bw. Vyagasa.

Bw. Vyagasa ametoa rai kwa Taasisi zote za Umma kuhakikisha kuwa mazingira ya kazi yanaboreshwa na watumishi wanapima afya zao mara kwa mara ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.