Baraza la wafanyakazi e-GA lajengewa uwezo

Na. Queenter Mawinda
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba, amewataka wajumbe wa Baraza kuendesha vikao vya Baraza kwa tija na ufanisi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo ya usimamizi na uendeshaji wa vikao hivyo.
Ndomba amesema hayo Novemba 21 mwaka huu jijini Dodoma, wakati akifungua kikao cha tatu cha Baraza la tano (5) la Wafanyakazi wa Mamlaka, kilichofanyika sambamba na mafunzo ya uendeshaji wa baraza hilo.
Alibainisha kuwa, ni wajibu wa kila mjumbe wa baraza kufahamu wajibu wake katika baraza na kuzingatia mafunzo yaliyotolewa ili kuwasilisha hoja zenye tija kwa wafanyakazi, taasisi na taifa kwa ujumla.
Aliwataka wajumbe hao kuendesha baraza kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kujadili mipango mbalimbali ya taasisi na kufanya tathmini ya ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yake.
“Ni matumaini yangu kuwa, baraza la mwaka huu litakuwa na tija zaidi na litaleta ustawi kwa taasisi kwa kuwa mmepata mafunzo yatakayowaongezea ufanisi katika uwasilishaji wa hoja mbalimbali za wafanyakazi, na hivyo mtaweza kujadili hoja hizo kwa uyakinifu zaidi ili kupata ufumbuzi wa changamoto hizo” alisisitiza Ndomba.
Naye Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE)) Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Sara Rwezaula, alimpongeza Mwenyekiti wa baraza kwa kufanya kikao cha tathmini ya utekelezaji wa bajeti, sambamba na mafunzo kwa wajumbe wa baraza ambayo amesema yataongeza ufanisi katika utekelezaji wa mipango mbalimbali iliyowekwa na Taasisi kwa maslahi mapana ya wafanyakazi na Taasisi kwa ujumla.

“Nawapongeza sana kwa kufanya kikao hiki cha tathmini, hii inaonesha ni kwa jinsi gani mmedhamiria kufikia malengo yenu na vipaumbele mlivyojiwekea kwa ustawi wa wafanyakazi na Taasisi” Alisema Bi. Rwezaula
Kikao cha tatu cha baraza la wafanyakazi kimewashirikisha wajumbe wa baraza kutoka Idara na Vitengo mbalimbali vya Mamlaka pamoja na wajumbe wa TUGHE Taifa na mkoa wa Dar es Salaam pamoja mwakilishi wa baraza Serikalini.



