Dkt. Kusiluka Awataka Maafisa TEHAMA Kusimamia Matumizi Salama ya Teknolojia kwa Maslahi ya Taifa

Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka, amewataka Maafisa TEHAMA nchini kutumia ujuzi wao ipasavyo na kusimamia matumizi sahihi ya teknolojia kwa maslahi mapana ya Taifa.
Dkt. Kusiluka ameyasema hayo wakati akifungua Kikao Kazi cha sita (6) cha Serikali Mtandao kilichofanyika tarehe 17–19 Februari, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), jijini Arusha.
Akizungumza katika kikao kazi hicho, Balozi Kusiluka alisema kuwa TEHAMA ni nyenzo muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma kwa umma, kuongeza uwazi na uwajibikaji Serikalini, pamoja na kuimarisha ukuaji wa uchumi wa kidijitali, hivyo matumizi bora ya teknolojia yanaweza kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi, kupunguza gharama na kuongeza ufanisi katika taasisi za umma.
Balozi Kusiluka alisema kuwa, kutokana na uwepo wa changamoto ya usalama wa kimtandao na matumizi ya teknolojia zinazochipukia ikiwemo akili unde, Maafisa TEHAMA wana wajibu wa kuhakikisha matumizi sahihi ya teknolojia hizi, kwa kutumia ujuzi wao kubuni na kusanifu mifumo kwa kuzingatia usalama wake, pamoja na kuhakikisha mifumo hiyo inakidhi viwango vinavyotakiwa kwa maendeleo ya nchi.
“TEHAMA ni kipaumbele cha Serikali na tayari hatua kubwa zimefikiwa. Hivyo, mnapaswa kusimamia matumizi ya teknolojia na kuhakikisha inatuletea maendeleo na siyo uharibifu,” alisisitiza.

Alisema ni matarajio yake kuwa Kikao kazi hicho kitakuja na maazimio ya namna ya kutumia teknolojia hizo zinazochipukia kwa uadilifu ikiwemo kuepuka matumizi hasi ya teknolojia yanayoweza kuhatarisha usalama wa taarifa na taifa kwa ujumla.
Aidha, Balozi Kusiluka ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kwa hatua kubwa iliyofikia ya utekelezaji wa agenda ya Serikali Mtandao, na kuzitaka taasisi zote za umma kufanyia kazi kwa haraka taarifa na mapendekezo yanayotolewa na e-GA pamoja na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ili kuimarisha uwajibikaji na ufanisi.
Vilevile, Balozi Kusiluka alizitaka Taasisi zote za Umma kuzingatia Sheria ya Serikali Mtandao ya Mwaka 2019, Kanuni, Viwango na Miongozo ikiwemo kuwasilisha andiko la miradi ya TEHAMA e-GA, kabla ya kuanzisha miradi hiyo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mha. Benedict Ndomba, alitaja mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na Mamlaka hiyo ikiwemo kuimarisha usimamizi wa miradi ya TEHAMA Serikalini na usimamizi na uendeshaji wa Mtandao wa Mawasiliano Serikalini (Government Network - GOVNET), hatua iliyochangia kupunguza urudufu wa mifumo, kuimarisha ubadilishanaji wa taarifa Serikalini baina ya mifumo ya taasisi mbalimbali pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma kwa kutumia TEHAMA.
Alisema hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050, kupitia lengo la kuhakikisha, zaidi ya asilimia 80 ya huduma za Serikali zinapatikana kupitia mifumo ya kidijitali iliyo salama na jumuishi ifikapo mwaka 2050.
Ndomba alimshukuru Katibu Mkuu Kiongozi kwa kufungua Kikao Kazi hicho, na kuahidi kusimamia utekelezaji wa maelekezo yote yalitolewa ili kuimarisha Utekelezaji wa Jitihada za Serikali Mtandao.
Kikao kazi cha sita (6) cha Serikali Mtandao kiliongozwa na Kaulimbiu iliyosema “Kuboresha Utendaji wa Serikali kwa Kuimarisha Utoaji wa Huduma za Umma Kupitia Mifumo Salama na Jumuishi ya Serikali Mtandao” ikiwa ina akisi dhamira ya Serikali ya kutumia mifumo ya kidijitali iliyo salama na jumuishi ili kuongeza ufanisi, tija, uwazi na uwajibikaji katika utendaji kazi, pamoja na kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.



