emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

e-GA NA MIKAKATI YA KUKUZA SERIKALI YA KIDIJITALI


e-GA NA MIKAKATI YA KUKUZA SERIKALI YA KIDIJITALI


Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imetaja mikakati mbalimbali iliyojiwekea ili kujenga Serikali ya kidijitali kwa kuhahikisha kuwa, Taasisi za Umma zinatoa huduma kwa wananchi kwa njia ya dijitali.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Meneja wa Usimamizi wa Uzingatiaji wa Viwango vya Serikali Mtandao wa Mamlaka Bi. Sultana Seiff, wakati akiwasilisha mada kuhusu Utoaji wa Huduma kwa Umma Kidijitali bila Kumuacha Mtu Nyuma (‘leaving no one behind in digital delivery of public service’) kwenye kongamano la 6 la TEHAMA lilifonyika katika Hoteli ya Golden Tulip iliyopo Zanzibar.

Bi. Sultana aliitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na Kuongeza uwezo wa rasilimali watu ili kusimamia utekelezaji wa mipango ya Serikali Mtandao, kushirikiana na wadau mbalimbali kutoka sekta za umma na binafsi katika kuimarisha ubunifu, ujenzi na usimamizi wa Mifumo ya TEHAMA ili kutoa huduma za umma kwa njia ya kidijitali pamoja na Kuhamasisha utafiti na ubunifu wa Serikali Mtandao kwa kushirikiana na Taasisi za Elimu ya Juu na zile za Utafiti.

“Ili kuimarisha Serikali Mtandao nchini, Mamlaka imejipanga kuhakikisha usalama wa mtandao kwa kudhibiti matishio yote ya usalama wa mtandao kwa kuyazuia au kuyaondoa pale yanapobainika pamoja na kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa katika Mifumo ya Serikali” alisisitiza Bi. Sultana na kuongeza kuwa,

Mamlaka imejipanga kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kusimamia uzingatiaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa Taasisi za Umma ili kujenga Serikali ya Kidijitali.

Kongamano la 6 la TEHAMA liliwakutanisha Zaidi ya wadau 600 wa TEHAMA kutoka ndani na nje ya nchi ili kujadiliana kwa pamoja na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya TEHAMA.

Tanzania Census 2022