emblem
Mamlaka ya Serikali Mtandao
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015
ega Logo
Habari
ega-svg-tree

Maafisa waandamizi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), wametakiwa kuimarisha waadilifu na kuzingatia vipaumbele vya taasisi na Serikali, ili waweze kuwa viongozi bora wa sasa na baadaye.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa e-GA, Mhandisi Benedict Ndomba, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uongozi yaliyofanyika hivi karibunimjini Morogoro.

Ndomba alisema, mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo Maafisa wakuu na waandamizi wa Mamlaka hiyo ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao, sambamba na kuongeza mchango katika kuleta mabadiliko chanya ndani ya taasisi.

“Mafunzo haya ni mojawapo ya juhudi endelevu za serikali, ili kuhakikisha Maafisa wakuu una waandamizi wanakuwa chachu ya mabadiliko katika taasisi, kwani wao ndio viongozi wa baadaye wa taifa hili,” alisema Ndomba.

Aidha, alieleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia washiriki kusimamia rasilimali watu kwa weledi, kuwa mfano wa kuigwa, na kuboresha utendaji wao wa kila siku. Alisisitiza kuwa uadilifu na weledi ni misingi isiyoweza kupuuzwa katika uongozi wowote unaotaka kufanikiwa.

Ndomba aliongeza kuwa, Mamlaka inatarajia kuona washiriki hao wakiwa na maarifa na mbinu za kisasa zaidi zitakazoongeza ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwa ni pamoja na kuwa viongozi wazuri kwa Maafisa walio chini yao mara tu baada ya kumaliza mafunzo hayo.

Kwa upande wake, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Bi. Jackline Jackson, ameishukuru Mamlaka kwa kuandaa mafunzo hayo akisema yatawasaidia kuwaongezea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi, kuongoza watu na kuongeza ufanisi wa utendaji katika taasisi.

“Mafunzo haya yatatusaidia kuongoza kwa kuzingatia kanuni, misingi ya maadili, uwajibikaji, haki na kufanya maamuzi ya kimkakati yenye manufaa kwa taasisi,” alisema Bi. Jackline.

Mafunzo hayo ya siku mbili, yalifanyika kuanzia Novemba 13 hadi 14 mjini Morogoro, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mamlaka unaolenga kuwaandaa Maafisa wakuu na waandamizi kuwa viongozi wa baadaye.

Mpangilio