emblem
Mamlaka ya Serikali Mtandao
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015
ega Logo
Habari
ega-svg-tree

Tanzania kupitia Mfumo wa e-Mrejesho toleo la pili (e-MrejeshoV2) imeibuka mshindi katika kipengele cha Serikali Mtandao, kwenyeTuzo za Mkutano wa Dunia wa Jumuiya ya TEHAMA mwaka 2025 (World Summit on the Information Society -WSIS 2025 grand winner).

Tuzo hizo ambazo huratibiwa na Shirika la Mawasiliano la Umoja wa Mataifa (International Telecommunications Union – ITU) zinalenga kutambua na kuchochea miradi bunifu, inayotumia TEHAMA katika kuchangia maendeleo endelevu duniani.

Akieleza kuhusu ushindi huo, Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bi. Subira Kaswaga amesema, Mfumo wa e-Mrejesho toleo la pili (V2), umeibuka mshindi wa tuzo hiyo katika kipengele cha Serikali Mtandao (e-Government AL C7), kati ya mifumo 360 ya TEHAMA iliyofuzu hatua ya mchujo kutoka kwa zaidi ya maombi 1000 ya mifumo ya kidijitali yaliyowasilishwa kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Meneja huyo amesema, e-GA ilipokea taarifa ya ushiriki wa tuzo mwishoni mwa mwezi Aprili, 2025 na kuwahamasisha wananchi kushiriki kupiga kura kwa wingi ili tuzo iweze kurudi nyumbani Tanzania.

“Nifuraha kubwa kuona wananchi wameweza kuitikia wito na kuwa wazalendo kwa kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha wanapiga kura kwa wingi na hatimaye tuzo imekuja nyumbani, kwa niaba ya e-GA tunawashukuru sana” amesema Bi. Subira.

Amebainisha kuwa, taarifa ya ushindi huo imepokelewa hivi karibunia kutoka ITU kupitia baruapepe na kuwa, tuzo hiyo itakabidhiwa rasmi kwenye Hafla ya Tuzo za WSIS 2025, itakayofanyika wakati wa Tukio la Ngazi ya Juu la Jukwaa la WSIS+20 (WSIS+20 Forum High-Level Event), mjini Geneva kuanzia tarehe 7 hadi 11 Julai mwaka huu.

Mfumo wa e-Mrejesho (V2) umesanifiwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) na kusimamiwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ukiwa umeboreshwa kwa kutumia teknolojia ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence - AI) katika kukusanya maoni ya wananchi.

Mfumo huu unapatikana kwa njia tatu ambazo ni kupitia simu ya mkononi kwa kubofya *152*00# na kisha kuchagua namba 8 na kisha namba 2 na kisha fuata maelekezo. Pia, kupitia simu janja kwa kupakua Aplikesheni tumizi (Mobile App) ya e-Mrejesho inayopatikana kwenye ‘Play Store na Apps Store’, na kwa njia ya Tovuti ya e-mrejesho.gov.go.tz.

Mpangilio