MAKALA: Mapinduzi ya Kidigitali Mahakamani: Hukumu sasa Zaandikwa kwa Akili Unde

Katika hatua inayotajwa kama mapinduzi ya kihistoria kwenye utoaji wa haki, Mahakama ya Tanzania imeanza kutumia Akili Unde (AI) katika uandishi wa hukumu, hatua inayorahisisha, kuharakisha na kuongeza uwazi wa mashauri huku ikiimarisha imani ya wananchi kwa mhimili huo wa dola.
Akizungumza katika Kikao Kazi cha sita cha Serikali Mtandao kilichofanyika jijini Arusha Februari 17 hadi 19, 2026, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel, amesema hukumu sasa zinaandikwa kwa kutumia teknolojia za kisasa.
“Kwa sasa hukumu zinaendeshwa kwa takwimu (data-driven). Tulitambua kuwa tunahitaji nguvu ya AI na matokeo yake yamekuwa ya kushangaza,” amesema Profesa Gabriel wakati akiwasilisha mada yake mbele ya Viongozi wa Taasisi za Umma, wataalamu wa TEHAMA na wadau kutoka ndani na nje ya nchi.
Ameeleza kuwa, Mwaka 2024 Mahakama ilianza majaribio ya Mfumo wa Kunukuu na Kutafsiri kwa njia ya sauti (Transcription and Translation Software - TTS), ambao tayari umejaribiwa katika kanda 11 za Mahakama nchini.
Kwa mujibu wake, mfumo huo umebadili kwa kiasi kikubwa namna hukumu zinavyoandikwa na kupunguza muda unaotumika.
“Zamani Jaji alikuwa anatumia muda mrefu kuandika hukumu yenye kurasa 200. Sasa Jaji anazungumza na mfumo unaandika moja kwa moja kwa Kiswahili au Kiingereza. Hii imeongeza ufanisi na pia inalinda afya na ustawi wa Majaji,” amefafanua.
Profesa Gabriel amesema, lengo kuu la matumizi ya AI na TEHAMA ni kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa wakati, kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa mashauri na kuimarisha uwazi katika utoaji wa huduma za Mahakama.
Amebainisha kuwa, mageuzi hayo tayari yameanza kuzaa matunda kwa kuongeza imani ya wananchi kwa Mahakama.
“Mwaka 2019 kiwango cha imani ya umma kwa Mahakama kilikuwa asilimia 70, lakini kufikia Mwaka 2023 kimeongezeka hadi asilimia 88,” amesema.

Mbali na uandishi wa hukumu, Mahakama imeimarisha pia ushirikiano wa kubadilishana taarifa na taasisi muhimu za umma zikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakala wa Usajili wa Leseni (BRELA), hatua inayorahisisha uratibu na utoaji wa huduma.
Akitolea mfano wa upana wa huduma za Mahakama nchini, alisema kwa kuwa Tanzania ina zaidi ya kata 3,956, matumizi ya teknolojia yanaisaidia Mahakama kuwafikia wananchi kwa ufanisi zaidi katika maeneo yote ya nchi bila kujali umbali wa kijiografia.
Amesisitiza kuwa mafanikio hayo hayawezi kupatikana bila uongozi imara na matumizi sahihi ya rasilimali.
“Kuwa na fedha ni jambo moja, kuzitumia kwa ufanisi ni jambo lingine,” amesisitiza, akiwataka watendaji wakuu kuwekeza kwa nguvu katika wataalamu wa TEHAMA kama mtaji wa kibinadamu, si rasilimali watu tu.
Kwa mujibu wa takwimu alizowasilisha, Mahakama kwa sasa inatekeleza zaidi ya programu 17, ambapo takribani asilimia 90 zinahusu maendeleo ya TEHAMA na rasilimali watu.
Miongoni mwa mageuzi makubwa yanayoendelea ni utekelezaji wa Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (Electronic Case Management System) unaolenga kuondoa matumizi ya mafaili ya karatasi na kuweka mfumo wa kidigitali.
“Sasa mwananchi anaweza kufungua kesi akiwa popote alipo, kufuatilia ni hakimu gani anashughulikia shauri lake na kunufaika na uwazi zaidi,” amesema.
Aidha, amebainisha kuwa TEHAMA imeongeza urahisi kwa mashahidi kutoa ushahidi kwa njia ya mtandao bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.
“Nani angeamini kuwa mtu aliyeko Canada anaweza kutoa ushahidi bila kuja Tanzania?” amehoji na kusisitiza kuwa mageuzi ya kidigitali ndani ya Mahakama lazima yaongozwe na uongozi thabiti ili kuhakikisha mabadiliko hayo yanakuwa endelevu na yenye tija kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Kikao kazi hicho kimekutanisha viongozi wakuu wa taasisi mbalimbali za umma, wataalamu wa TEHAMA na wadau wa maendeleo kutoka nchi tofauti, ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa zikionesha namna Tanzania inavyoendelea kuwekeza katika teknolojia ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utumishi wa umma



