emblem
Mamlaka ya Serikali Mtandao
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015
ega Logo
Habari
ega-svg-tree

Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA Serikalini, wametakiwa kuzifanyia kazi hoja mbalimbali zinazoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu mifumo ya TEHAMA ili kuhakiksha hoja hizo hazijirudii.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba, wakati wa mafunzo ya siku tatu ya Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA kutoka ofisi za Makatibu Tawala Mikoa ya Tanzania Bara na Halmashauri zote nchini. 

Amesema kuwa, yapo maeneo ambayo CAG ameyagusa na kuyatangaza katika ripoti ya Ukaguzi wa mifumo ya TEHAMA hivyo ni jukumu la Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA Serikalini, kuhakikisha wanazipitia na kuzifanyia kazi hoja zote zinazowagusa ili zisijirudie.

“Nia kubwa ya kufanya hivi ni kuhakikisha tunaboresha utendaji kazi wetu, na kuhakikisha mifumo ya TEHAMA tunayoianzisha au kuisimamia inakidhi matarajio ya serikali katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi,” amefafanua Mha.Ndomba.

Sambamba na hilo, Ndomba amewataka viongozi hao kuhakikisha kila mtumishi wa umma katika taasisi husika anakuwa na baruapepe ya serikali, ili awezeshwe kuifikia mifumo mbalimbali ya Serikali.

“Kuna mifumo ya kiutendaji ambayo inamlazimu mtumishi wa umma kuwa na baruapepe ya Serikali ili aweze kuitumia mifumo hiyo, ukiwemo mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office), hivyo ni muhimu kuhakikisha watumishi wote katika taasisi zenu wanazo baruapepe za serikali ili waweze kutekeleza majukumu yao,” amesema Ndomba.

Mafunzo hayo ya siku nne yalifanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Dodoma mwezi April  mwaka huu na kuratibiwa na e-GA kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, UTUMISHI pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

 

Mafunzo hayo, yalilenga kuwajengea uwezo Wakuu wa vitengo vya TEHAMA kutoka ofisi za Makatibu Tawala Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na wengine kutoka Halmashauri mbalimbali nchini, katika maeneo ya Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao.

Mpangilio