emblem
Mamlaka ya Serikali Mtandao
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015
ega Logo
Habari
ega-svg-tree

Maafisa Habari Serikalini, wametakiwa kuzingatia weledi katika uandaaji na utoaji wa taarifa za Serikali kupitia tovuti za taasisi, ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu shughuli na miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali kupitia tovuti hizo.

Wito huo umetolewa Novemba 18 mwaka huu, na Mkurugenzi wa Huduma za Uwezeshaji wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Bw. Erick Kalembo, wakati akifungua mafunzo ya Usimamizi na Uendeshaji wa Tovuti za Serikali, kwa Wakuu wa Vitengo vya Habari na Mawasiliano Serikalini, pamoja na Maafisa Habari wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya.

Bw. Kalembo alisema kuwa, sekta ya afya imebeba uhai wa wananchi na hivyo ni muhimu kwa Maafisa Habari kuhakikisha wanahuisha na kuweka taarifa sahihi kwenye tovuti, ili kuwawezesha wananchi kupata taarifa na elimu muhimu kuhusu masuala mbalimbali ya afya, pamoja na kufahamu jitihada zinazozifanywa na Serikali, katika kuimarisha sekta ya afya.

 “Maafisa Habari mmepewa dhamana kubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi zinazohusu Serikali, ikiwemo miradi ya maendeleo, lakini ninyi mliopo sekta ya afya mnayo dhama lubwa zaidi ya kulinda na kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala ya afya ikiwemo magonjwa ya milipuko kwa kuweka taarifa sahihi katika tovuti”, alisema Kalembo.

Aliongeza kuwa, jukumu la Maafisa Habari ni pamoja na kufanya uchambuzi yakinifu wa taarifa kwa kuzingatia misingi na weledi wa uandishi wa habari, kabla ya kuziweka kwenye tovuti kwa maslahi mapana ya taifa.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa wataalamu hao kuwasiliana na e-GA mara wanapokutana na changamoto zozote za kiufundi katika upandishaji wa taarifa kwenye tovuti wanazozisimamia, ili kupata ufumbuzi na kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata taarifa sahihi kwa wakati.

“Kwa kuzingatia kasi ya mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia, ni muhimu kuboresha tovuti zenu mara kwa mara kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo mbalimbali inayosimamia tovuti za Serikali, ukiwemo Mwongozo wa Usimamizi na Uendeshaji wa Tovuti za Serikali wa mwaka 2014 na Mwongozo wa Matumizi Bora, Sahihi na Salama wa Vifaa, Data na Mifumo ya TEHAMA Serikalini wa mwaka 2022”, alisisitiza Bw. Kalembo.

Kwa upande wake, Bi. Rozina Suka, Afisa Habari Mwandamizi wa Hospitali ya Tumbi na mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, ameipongeza e-GA kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yalilenga kuwajengea uwezo wa kusimamia na kuendesha tovuti za Serikali, pamoja na kuwapatia uelewa kuhusu Sheria ya Serikali Mtandao ya mwaka 2019.

Katika mafunzo hayo, mada mbalimbali ziliwasilishwa zikiwa na lengo la kuongeza uwezo wa Maafisa Habari katika usimamizi wa maudhui na kuimarisha weledi katika utoaji wa taarifa kupitia tovuti pamoja na nafasi ya Maafisa Habari katika kuimarisha na kujenga Serikali Mtandao.

Mada hizo zilijumuisha Sheria ya Serikali Mtandao, matumizi ya teknolojia zinazoibukia, usalama wa tovuti, na usimamizi wa mitandao ya kijamii ili kuwawezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimtandao.

Mafunzo hayo ya siku nne yalifanyika kuanzia Novemba 18 hadi 21, mwaka huu mkoani Morogororo. Mafunzo hayo ni mkakati wa e-GA wa kuwajengea uwezo Maafisa Habari Serikalini katika kuimarisha utoaji wa taarifa za Serikali kupitia tovuti.

Mpangilio