emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

IMARISHENI UADILIFU KAZINI: MHANDISI NDOMBA


IMARISHENI UADILIFU KAZINI: MHANDISI NDOMBA


Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), wametakiwa kuimarisha na kuendeleza uadilifu kazini ili kuhakikisha Mamlaka inatekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi zaidi.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Mhandisi Benedict Ndomba Februari 26 mwaka huu, wakati akifungua kikao cha wafanyakazi wa Mamlaka kilichofanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa, ili Mamlaka iendelee kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa ni lazima watumishi wake wawe na weledi na uadilifu wa kutosha katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

“Natambua kuwa, mmekuwa mkizingatia weledi na uadilifu katika kazi zenu lakini hiyo haitoshi, ni lazima muhakikishe mnaimarisha zaidi weledi na uadilifu mlionao sasa, ili kwa pamoja tuweze kufikia malengo ya taasisi tuliyojiwekea,” alisema Mhandisi Ndomba.

Aliongeza kuwa, uimara wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA Serikalini inayosimamiwa na Mamlaka hiyo hutokana na uadilifu wa watumishi na hivyo, hatari huweza kutokea ikiwa watumishi hao watakosa uadilifu.

“Tunafahamu kuwa matishio ya kiusalama mtandaoni hutokea kila mara duniani kote, ni lazima tuendelee kuyadhibiti ili kulinda mifumo na miundombinu ya TEHAMA tunayosimamia, tunaweza kufanikiwa ikiwa sote tutaendelea kuwa waadilifu,” alisisitiza Mhandisi Ndomba.

Naye Mkurugenzi wa Huduma na Uwezeshaji wa Mamlaka hiyo CPA. Bw. Salum Mussa alisema, Mamlaka itaendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wote ili kuendelea kuimarisha utendaji kazi wa Mamlaka.

“Mamlaka itaendelea kuwajengea uwezo watumishi wake kwa kutenga fedha kwa ajili ya mafunzo mbalimbali ili kuimarisha ujuzi na kuendana na mabadiliko ya teknolojia yanayotokea kila siku,” alisema CPA. Bw. Salum Mussa.

Aliongeza kuwa, nia ya Mamlaka ni kuhakikisha kila mtumishi anaendeleza ujuzi alionao kwa kupata mafunzo mara kwa mara kutokana na mahitaji yatakayojitokeza na kuwasihi watumishi kutumia vema fursa hiyo kwa maslahi mapana ya taasisi.

Kwa upande wa watumishi wa Mamlaka walioshiriki kikao hicho, waliupongeza uongozi kwa kuandaa kikao ambacho kiliwakutanisha watumishi wote kwa pamoja na kupata elimu kuhusu mambo mbalimbali yakiwemo afya na uwekezaji.

“Kikao hiki kimekuwa na manufaa makubwa kwani, tumejifunza kuhusu afya ya akili, uwekezaji na masuala ya rushwa kutoka kwa wataalamu wa maeneo hayo, lakini pia tumeona mipango ya taasisi katika kutuendeleza watumishi wake,” alisema Bw. Jacob Willy, Afisa TEHAMA Mwandamizi wa e-GA.

Naye Bi. Sara Mgale Afisa Ugavi wa Mamlaka aliipongeza e-GA kwa kutenga bajeti ya mafunzo kwa watumishi wake kila mwaka, ili kuhakikisha wanaendeleza na kuimarisha ujuzi wao, hali ambayo imechangia kuongezeka kwa weledi hivyo kuongeza ufanisi kwenye utendaji kazi katika Idara na Vitengo.

Kikao cha watumishi wa Mamlaka kilifanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia Februari 26 hadi 28 mwaka huu, ambapo mada mbalimbali zilizohusu afya, uwekezaji, maadili ya utumishi wa umma pamoja na rushwa, ziliwasilishwa na baadaye kikao hicho kilihitimishwa kwa bonanza la michezo lililofanyika katika viwanja vya Gymkhana.