emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YAIPONGEZA e-GA


KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YAIPONGEZA e-GA


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) imeipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kuendelea kusimamia na kubuni mifumo tumizi ya TEHAMA ambayo inarahisisha utendaji kazi wa Serikali katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Pongezi hizo zimetolewa leo katika Ofisi za Bunge Jijini Dodoma, mara baada ya Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mhandisi Benedict Ndomba kuwasilisha mada kuhusu Usalama wa Serikali Mtandao mbele ya kamati hiyo iliyolenga kuwajengea uwezo viongozi hao kuhusu usalama wa mitandao.

“Mimi niipongeze sana e-GA kwa ubunifu wa mifumo mbalimbali ya Serikali, miongoni mwa mifumo hiyo ni Mfumo wa Ukusanyaji Malipo ya Serikali kwa njia ya Mtandao (GePG) kwani, umesaidia katika ukusanyaji wa fedha za Serikali na kupunguza ubadhilifu pia sasahivi unaweza ukalipa maji au umeme muda wowote kupitia mfumo wa MAJIS,hongereni sana’’ alisema Mh. Dkt.Thea Ntala Mjumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mh. Abdallah Chaurembo ameeleza kuridhishwa na utendaji kazi wa e-GA na kueleza kuwa miongoni mwa mifumo mizuri iliyobuniwa na e-GA ni mfumo wa e-Mrejesho ambao unasaidia wananchi kuwasilisha maoni au malalamiko yao sambamba na kuweza kufuatilia ili kupata majibu sahihi kutoka katika taasisi husika

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa eGA Mhandisi Ndomba amewasisitiza wabunge na wananchi kwa ujumla kuwa makini ili kuepuka udukuzi wa taarifa zao pindi wanapotumia vifaa vya kielektroniki kama vile vishikwambi, kompyuta na simu za mkononi, ikiwa ni pamoja na kutofungua viunganishi (links) wanazotumiwa bila ya kuzielewa vizuri ili kujiepusha kudukuliwa kwa taarifa zao.

Eng. Ndomba ameeleza kuwa, wadukuzi wa taarifa mitandaoni hutumia mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutuma ‘links’ zisizokuwa sahihi na kutumia majina ya watu maarufu kama vile viongozi kwa lengo la kuwahadaa wananchi na kisha kudukua taarifa zao.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Jenista Mhagama, ameipongeza e-GA kwa weledi na ubunifu katika utendaji kazi wake na kuitaka kuongeza juhudi zaidi katika kubuni na kutengeneza mifumo tumizi ya TEHAMA inayotatua changamoto mbalimbali zilizopo katika mazingira yetu.