emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

Mahakama ya Tanzania kutumia Mfumo wa Ofisi Mtandao katika Utendaji kazi


Mahakama ya Tanzania kutumia Mfumo wa Ofisi Mtandao katika Utendaji kazi


Mahakama ya Tanzania imejipanga kuanza rasmi matumizi ya Ofisi Mtandao (e-Office) kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi na kuhakikisha kuwa ndoto ya kuwa Mahakama Mtandao (e-Judiciary) inatimia.

Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel Katika kikao chake cha kwanza na Menejimenti ya Mahakama kilichofanyika Agosti 23, 2021. Kikao hiki ni cha kwanza na Menejimenti baada ya kuteuliwa na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania agosti 21, 2021 Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Prof. Elisante alifafanua masuala mbalimbali kwa menejimenti hiyo ikiwa ni pamoja na dhamira yake ya matumizi ya TEHAMA mahakamani ambapo alielekeza kuwa ifikapo Septemba mosi, mwaka huu Mfumo wa Ofisi Mtandao unatakiwa kuanza kufanya kazi.


Akizungumza katika mahojiano maalum Agosti 31, 2021 yaliyolenga kufahamu hatua zilizofikiwa katika maandalizi ya kuanza kutumika kwa Ofisi mtandao, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Kumbukumbu-Mahakama ya Tanzania, Bi. Agnes Bulyota amebainisha kuwa maandalizi yako na kesho Septemba 01, 2021 Mahakama itaanza kutumia mfumo huo katika ngazi ya Makao Makuu ya Mahakama, Mahakama ya Rufani pamoja na Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni.

“Mahakama inaendelea na maboresho ya utendaji kazi ikiwamo kuongeza kasi katika utoaji uamuzi. Kwa hiyo tumeamuwa kuungana na baadhi ya Wizara na Taasisi za Serikali zaidi ya 100 ambazo zinatumia Ofisi Mtandao” alisema Bi. Agnes.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa, mpango wa Mahakama ni kuhakikisha kuwa mfumo huu unatumika katika ngazi zote za Mahakama nchini, ambapo ameeleza kuwa kwa upande wa Mahakama Kuu-Masjala Kuu, Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wataanza mafunzo ya Ofisi mtandao Septemba 02 mwaka huu ili kujiweka tayari kwa ajili ya kuanza matumizi ya mfumo huo.

“Zoezi hili litakuwa likifanyika kwa awamu ili kuhakikisha kuwa Mahakama nzima inatumia mfumo huu, vilevile mafunzo tajwa yamepangwa kutolewa pia kwa Watumishi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki nchini (IJCs) ili nao waweze kutumia mfumo huu katika majengo hayo mapya ya Mahakama,” alieleza.

Mkurugenzi huyo ameainisha faida za matumizi ya mfumo huo ikiwa ni pamoja na kurahisisha utendaji kazi kwa kutumia TEHAMA kwa kuwa taarifa zote muhimu za kufanyia kazi zinawekwa kiielektroniki, kuongeza ufanisi wa kazi, kuongeza kasi ya kufanya maamuzi kwa wakati, kupunguza matumizi ya karatasi na kudhibiti matumizi mabaya ya taarifa za kiofisi.

Mbali na mfumo huu, Mahakama ina mifumo ya TEHAMA kadhaa ikiwemo Mfumo wa Kusajili na kuratibu mashauri kwa njia ya Kieletroniki (JSDS), ‘TAMs’ na mingineyo yote ikilenga katika kumrahisishia mwananchi kupata huduma ya haki kwa wakati.

Mfumo huu wa Ofisi Mtandao ‘e-office’ umesainifiwa na mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kushirikiana na Idara ya Nyaraka na Kumbukumbu za Taifa (RAMD) ambao wanasimamia taratibu na mifumo ya Masjala nchini.

Tanzania Census 2022