emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

MAJIIS: MFUMO UNAOZIUNGANISHA MAMLAKA ZA MAJI NCHINI


MAJIIS: MFUMO UNAOZIUNGANISHA MAMLAKA ZA MAJI NCHINI


Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa kushirikiana na Wizara ya Maji imesanifu na kutengeneza Mfumo wa Pamoja wa Utoaji Ankara za Maji (Maji Intergrated and Unified Billing System-MAJIIS) kwa lengo la kurahisisha uendeshaji, usimamizi na udhibiti wa mapato ya Mamlaka za Maji na Bodi za maji za Mabonde Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mhandisi. Benedict Ndomba amesema kuwa, awali taasisi nyingi za maji hazikuwa na mifumo inayorahisisha utendaji kazi na baadhi ya taasisi zilikuwa na mifumo ambayo haikuwasiliana.

Hali hiyo ilipelekea upatikanaji wa taarifa za wateja pamoja na makusanyo kuchukua muda mrefu na wakati mwingine taarifa hizo hazikuwa sahihi na hivyo Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Mamlaka ikatengeneza mfumo wa MAJIIS ili kutatua changamoto hizo.

“Mfumo huu ni muhimu kwa taasisi za maji kwani umerahisisha utoaji huduma na ukusanyaji mapato kufanyika kwa ufanisi zaidi pia, utoaji wa huduma kwa umma umerahisishwa kwa kuwezesha ulipaji wa ankara za maji kufanyika kwa wakati na mahali popote, kwa kutumia vitumi vya kielektroni kama kompyuta na simu za mkononi” amesema Mhandisi Ndomba.

Aidha, Mhandisi Ndomba amezihimiza Mamlaka za Maji pamoja na Bodi za Maji za Mabonde ambazo bado hazijaunganishwa kwenye mfumo huo kufanya jitihada za makusudi za kuunganishwa katika mfumo ili kuondoa kero mbalimbali kwa wananchi.

Akifafanua kuhusu mfumo huo Meneja wa Kitengo cha Huduma za Serikali Kupitia Simu za Mkononi wa Mamlaka Bw. Abdallah Samizi amesema kuwa, mfumo huo umeleta ufanisi, uwazi, na umesaidia kupunguza mianya ya rushwa kwa kuondoa ulazima wa mteja na mtoa huduma wa taasisi ya maji kukutana ana kwa na ili kupata huduma.

“Kwa sasa mteja anaweza kujihudumia mwenyewe kupitia simu yake ya mkononi kwa kupiga namba *152*00#, atachagua namba 6 Maji, kisha 1 Huduma za pamoja za maji ambapo atakutana na orodha inayoonesha huduma mbalimbali za maji na atachagua kadiri ya hitaji lake” amesema Bwa.Samizi.

“Mfumo wa MAJIIS unasaidia kufanya tathmini ya matumizi ya maji ya mteja katika vipindi tofauti vya matumizi na kumuhakikishia mteja kupata ankara ya maji sahihi kutokana na matumizi yake”

Bwana Samizi amefafanua kuwa MAJIIS ni mfumo shirikishi na umetengenezwa kwa lengo la kuziwezesha Mamlaka za Maji kuendesha shughuli zao katika mfumo mmoja.

Aidha, ameongea kuwa mfumo huo unaruhusu Maafisa mbalimbali wa Taasisi pamoja na Afisa Masuuli pamoja na Maafisa wengine wa Taasisi kufuatiliataarifa za usomaji wa dira za wateja zinazokusanywa na watendaji katika ngazi mbalimbali, vilevile unatoa uwezo wa kuhakiki taarifa hizo kabla ya ankara ya maji kumfikia mteja.

“Mfumo wa MAJIIS unasaidia kufanya tathmini ya matumizi ya maji ya mteja katika vipindi tofauti vya matumizi na kumuhakikishia mteja kupata ankara ya maji sahihi kutokana na matumizi yake”