emblem
Mamlaka ya Serikali Mtandao
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015
ega Logo
Habari
ega-svg-tree

Mkurugenzi wa Udhibiti na Usalama wa TEHAMA Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bw. Sylvan Shayo, amesema matumizi ya mifumo ya TEHAMA Serikalini, yameimarisha uwazi na ufanisi kwakuwa,  Serikali  inao uwezo mkubwa wa kuhifadhi nyaraka, na kupata kumbukumbu kwa usahihi na kwa wakati. 


Bw.Shayo ameyasema hayo Agosti 26, mwaka huu jijini Dar es Salaam, wakati akiwasilisha  mada kuhusu  matumizi ya Ofisi Mtandao ndani ya sekta za Umma, katika kikao cha 13 cha Wataalam wa  Kumbukumbu na Nyaraka, kilichoandaliwa na Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania  (TRAMPA).

Alisema kuwa, mapinduzi hayo yamechangiwa na uwepo wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo bora ya Serikali Mtandao.

 “Leo taasisi zaidi ya 380 zinatumia mifumo ya kielektroniki kuhifadhi kumbukumbu na kuwezesha utoaji wa huduma kwa haraka na kuondoa urasimu, lakini pia kwa sasa faili haziwezi kupotea wala kughushiwa kirahisi kwa sababu, taarifa zinapatikana moja kwa moja kutoka kwenye vyanzo rasmi”, alifafanua Shayo.


Aliongeza kwamba, TEHAMA imewezesha taarifa muhimu kuhifadhiwa na kufikiwa kwa urahisi bila kuhitaji mtu kuzibeba au kuzisafirisha kutoka sehemu moja hadi nyingine, aidha Kumbukumbu na Nyaraka muhimu sasa zinapatikana kidijitali, hali inayopunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya kughushi au kupotea kwa majalada ya Serikali. 


Shayo alisema, TEHAMA imeboresha utendaji kazi katika sekta mbalimbali zikiwemo sekta za ardhi, elimu na afya kuanzia uombaji na utoaji wa hati miliki za ardhi, matokeo ya mitihani hadi taarifa za wagonjwa.
 
“TEHAMA inatulazimu kuongeza uwajibikaji, kasi na uwazi wa kweli katika utoaji wa huduma kwa umma", alisisitiza Bw. Shayo.

Mkutano huo uliongozwa na kauli mbiu isemayo “Matumizi ya Ofisi Mtandao ni Chachu ya kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 – 2050” uliwakutanisha Maafisa Kumbukumbu zaidi ya 1000 kutoka katika taasisi mbalimbali za Umma.

Mpangilio