emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

MFUMO IMARA WA UKAGUZI CHACHU YA MABADILIKO KATIKA UTENDAJI KAZI


MFUMO IMARA WA UKAGUZI CHACHU YA MABADILIKO KATIKA UTENDAJI KAZI


Utekelezaji wa Jitihada za Serikali Mtandao unategemea uwepo wa mfumo imara wa ukaguzi utakaoboresha na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika kaguzi mbalimbali zinazofanywa na wakaguzi ndani na nje ya Taasisi za Umma.

Mfumo mpya wa ukaguzi ujulikanao kama e-Ukaguzi ni mfumo unaosaidia na kuimarisha utendaji kazi wa kaguzi za ndani za Taasisi za Umma ikiwemo kuandaa mpango kazi wa mwaka, kufanya ufuatiliaji wa hoja mbalimbali za kikaguzi ndani na nje ya Taasisi pamoja na kufanya uchambuzi wa vihatarishi vikubwa katika maeneo yote ya Taasisi yanayokaguliwa.

Mfumo huu jumuishi ni matokeo ya ubunifu uliofanywa na wazawa kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao katika kuhakikisha kuwa matumizi ya TEHAMA Serikalini yanaimairishwa na huduma mbalimbali zitolewazo kwa Wananchi zinaboreshwa.

Meneja wa Kituo cha Utafiti na Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGovRIDC) Mamlaka ya Serikali Mtandao Bw. Jaha Mvulla amesema kuwa lengo la kuanzishwa kwa mfumo huu lilikuwa ni kurahisisha utendaji kazi kwa wakaguzi wa ndani, kupunguza matumizi ya karatasi, kuongeza ufanisi na kutunza muda wa kufanya kaguzi mbalimbali.

Aidha, Bw. Jaha amesema kuwa mfumo huu unaruhusu wakaguzi wa ndani kupanga, kutekeleza na kufuatilia matokeo ya kaguzi, unachakata na kurahisisha upatikanaji wa ripoti mbalimbali kama za mwaka, mwezi, n.k.

Pia Bw. Jaha amesema mfumo huu umewapa uwezo Wakuu wa Idara kujibu kila hoja zitokanazo na kaguzi zote zinazohusu Idara zao.

“Mfumo unatoa nafasi kwa Wakaguzi wa Ndani kuweka na kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa hoja za kaguzi za nje ya Taasisi kama zile za CAG, PPRA, OSHA, BOT na nyinginezo zinazohusu utendaji wa Taasisi hizo” Alisema Bw. Jaha

Bw Jaha ameongezea kuwa Mamlaka ya Serikali Mtandao ilisanifu mfumo huu kutokana na uhitaji mkubwawa kutaka kuboresha na kuongeza ufanisi wa kazi mbalimbali za kaguzi za Taasisi za Umma wakati wa kuandaa mpango kazi ili kuhakikisha kuwa kaguzi zote zinazofanyika zinakuwa na tija kwa Taasisi.

Bw. Jaha ametoa wito kwa Taasisi za Umma na Halmashauri mbalimbali nchini kutumia mfumo huu mpya wa ukaguzi katika utekelezaji wa kaguzi mbalimbali na ufuatiliaji wa hoja zinazotokana na kaguzi hizo ndani na nje ya Taasisi zao.

Itakumbukwa kuwa hivi karibuni Mamlaka ya Serikali Mtandao ilitoa mafunzo maalum ya ukaguzi wa Mifumo na Miradi ya TEHAMA kwa Wakaguzi wa Ndani wa Halmashauri na Tawala za Mikoa 13 za Tanzania Bara walioshiriki katika mafunzo ya siku tano mkoani Morogoro.

Mafunzo hayo yalilenga kuwawezesha na kuwajengea uwezo Wakaguzi wa Ndani kukagua Mifumo na Miradi ya TEHAMA ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuisaidia Serikali kuona thamani halisi ya fedha ilizowekeza katika miradi na mifumo ya TEHAMA.