emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

MFUMO WA e-Mrejesho WASHINDA TUZO YA UMOJA WA MATAIFA YA UBUNIFU KATIKA HUDUMA ZA UMMA


MFUMO WA e-Mrejesho WASHINDA TUZO YA UMOJA WA MATAIFA YA UBUNIFU KATIKA HUDUMA ZA UMMA


Tanzania imeshinda tuzo ya Umoja wa Mataifa ya Ubunifu katika Huduma za Umma kwa mwaka 2024 ‘UN Public Service Innovation Awards’ kupitia mfumo wa e-Mrejesho, ambao umetambuliwa na umoja huo kama jukwaa linalowezesha serikali kukusanya maoni na malalamiko ya wananchi kwa njia ya kidijitali, na hivyo kufanya maamuzi ya sera na utekelezaji kwa wakati.

Hafla ya utoaji wa tuzo za Umoja wa Mataifa kuhusu Huduma za Umma imefanyika Juni 26 mwaka huu wakati wa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ya Umoja wa Mataifa ‘UN Public Service Week 2024’ katika jiji la Incheon, Jamhuri ya Korea.

Tanzania ilikuwa moja kati ya nchi mbili tu za Afrika zilizotunukiwa tuzo hiyo, nyingine ikiwa ni Afrika Kusini ambapo jumla ya nchi 73 wanachama wa Umoja wa Mataifa zilishiriki na mifumo 400 iliwasilishwa wakati mifumo 15 pekee ndiyo ilishinda tuzo mbalimbali ukiwemo mfumo wa e-Mrejesho.

Tuzo hizo zilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Idara ya Masuala ya Kiuchumi na ya Kijamii Bw. Li Junhua, pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Korea, Bw. Lee Sang-min, na kupokelewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi.

Mfumo wa e-Mrejesho umesanifiwa na kutengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, unaruhusu wananchi kuwasiliana na taasisi zote za Serikali na kuwasilisha maoni, malalamiko au pongezi.

Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mhandisi Benedict Ndomba amesema kuwa, tuzo hiyo inaonesha utambuzi wa mchango mkubwa wa mfumo wa e-Mrejesho duniani kama jukwaa huru linalowaunganisha wananchi na serikali katika kuboresha utawala wa demokrasia kupitia teknolojia.

Amebainisha kuwa, mfumo huu unaruhusu Serikali kukusanya malalamiko, maswali na maoni ya wananchi na kuyafanyia kazi kwa wakati na pia unamuwezesha mwananchi kutuma maoni yake bila kujulikana ikiwa mwananchi hatotaka kujulikana.

“Mfumo wa e-Mrejesho ni jukwaa huru kwani umezingatia faragha za wananchi ambapo kwa wale wasiopenda kujulikana wanapowasilisha maoni yao serikalini wanaweza kuwasilisha bila kujulikana, na hivyo kuhakikisha sauti za watu zote zinasikilizwa, hii inachochea utamaduni wa uwazi na uwajibikaji katika taasisi za umma”, amesema Ndomba.

Ameongeza kuwa, mfumo wa e-Mrejesho ni hatua kubwa katika juhudi za e-GA za kujenga daraja kati ya serikali na wananchi wake na kuwa, ushindi wa tuzo hio kutoka kwa Umoja wa Mataifa unaonesha namna azma ya e-GA ya kukuza uwazi na uwajibikaji katika utawala wa umma kupitia teknolojia inavyotekelezwa.

“Mfumo wa e-Mrejesho unapatikana kwa njia tatu ambazo ni kupitia simu ya mkononi kwa kubofya *152*00# na kisha kuchagua namba 9 na kisha namba 2, njia zingine ni kupitia simu janja kwa kupakua Aplikesheni (Mobile App) ya e-Mrejesho inayopatikana kwenye Play Store na Apple Apps Store, na kwa njia ya Tovuti ya emrejesho.gov.go.tz”, amesema Ndomba.

Aidha, amebainisha kuwa, ikiwa mwananchi atakosea kuwasilisha lalamiko lake katika taasisi husika, mfumo wa e-Mrejesho unaruhusu lalamiko hilo kuhamishwa kutoka taasisi moja kwenda taasisi nyingine, na pia unamruhusu mwananchi kukata rufaa kwenda ngazi ya juu ya taasisi ikiwa hatoridhika na majibu yaliyotolewa kuhusu lalamiko lake.

Mfumo huu unasaidia kuongeza uwajibikaji, kwani lalamiko linapofika kwenye taasisi litaonekana kwenye ngazi zote za uongozi wa taasisi hiyo na kila Afisa aliyelifungua ama kulifanyia kazi ataonekana, pia mfumo unafanya uchambuzi wa taarifa na kumuwezesha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais UTUMISHI na Katibu Mkuu Kiongozi kuona malalamiko yaliyowazi, yanayoshugulikiwa na yaliyokamilika kupitia ‘dashboard’ maalum”, amesema Ndomba.

Machi 13 mwaka huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan, aliwataka viongozi wa umma kutumia Mfumo e-Mrejesho ili kupokea maoni ya wananchi kuhusu Serikali na pia kutoa mrejesho kwa wananchi kupitia mfumo huo ili kuimarisha uwajibikaji kwa viongozi wa umma.

Dkt. Samia alitoa maelekezo hayo Ikulu jijini Dar es Salaam, mara baada ya kuwaapisha viongozi aliowateua katika nafasi mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Katibu Mkuu, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri.

Tuzo za Umoja wa Mataifa kuhusu Huduma za Umma zinalenga kuhamasisha ufanisi, uwazi na ushirikishwaji katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, na kuthamini mchango wa taasisi za umma katika kukabiliana na mahitaji ya kijamii, kiuchumi na mazingira ya jamii.

Wiki ya Huduma ya Umma ya Umoja wa Mataifa ni tukio la kila mwaka, linaloadhimishwa kimataifa kwa lengo la kusherehekea thamani na umuhimu wa huduma ya umma kwa jamii na hujadili jinsi ya kuboresha utoaji wa huduma kwa umma duniani kote.